1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya Wahariri juu ya Romney

Wahariri wanauzungumzia mkutano mkuu wa chama cha Republican na ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini China.

Mgombea urais wa chama cha Republican,Mitt Romney na Mkewe

Mgombea urais wa chama cha Republican Mitt Romney na Mkewe

Mhariri wa gazeti la "Sächsische" anatoa maoni yake juu ya mkutano mkuu wa chama cha Republican baada ya wajumbe wa chama hicho kumteua Mitt Romney kuwa mgombea urais kwa niaba ya chama chao.

Mhariri huyo anasema jambo linaloweza kuwa la muhali kwa Mitt Romney ni mpango wake unaoweza kusababisha mvutano na wahafidhina wa chama chake, kuhusu masuala ya utoaji wa ujauzito,haki ya kumiliki silaha na mageuzi katika mfumo wa afya. Wahafidhina hawapo tayari kuvumilia udhaifu juu ya masuala hayo. Na mjumbe asiekuwa na msimamo thabiti,wakati wote atapwaya wakati wa uchaguzi katika nchi kama Marekani ambapo wananchi wanamtaka Rais wao aonyeshe ukakamavu katika uongozi.

Mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anasema udhaifu wa Romney utakuwa na maana ya ushindi kwa Obama. Gazeti hilo linasema Romney atakuwa na uwezekano wa kushinda,ikiwa uchumi wa Marekani utaendelea kudhoofika hadi wakati wa uchaguzi.

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linatilia maanani kwamba tabaka la kati nchini Marekani linatatizika. Katika upande mmoja linamwona Romney kuwa ni mtaalamu wa uchumi.Lakini katika upande mwingine halipo tayari kumtelekeza Obama. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa tabaka la kati nchini Marekani linataka kuijua programu ya Romney.Jee anakusudia kufanya nini, kwa manufaa mwanachi wa kawaida? Pamoja na nderemo zote kwenye mkutano mkuu wa chama cha Republican, Tampa Florida jambo moja haliwezi kufichika.Kwamba Romney bado hajazifikia nyoyo za tabaka la kati nchini Marekani.

Kansela wa Ujerrumani Angela Merkel anahudhuria kikao kingine cha mashauriano baina ya serikali za Ujerumani na China kinachofanyika mjini Beijing. Lakini gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" linasema katika maoni yake kwamba vikao kama hivyo siyo mbadala wa kuuonyesha wazi msimamo wa Ujerumani juu ya masuala ya utatanishi baina yake na China.Mhariri wa gazeti hilo anasema uelewano ukizidi sana baina ya China na Ujerumani , siyo jambo zuri sana.Kwa sababu madaha ya itifaki yanayohusu mashauriano baina ya serikali za nchi hizo mbili hayawezi kuchukua mahala pa kuambikiana ukweli.Yapo masuala ya utatanishi baina ya Ujerumani na China.Pamoja na hayo ni kubaguliwa kwa kampuni za Ujerumani. Na pia pana suala la kubanwa kwa haki za binadamu,utawala wa kisheria na kubwana kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Mwandishi:Mtullya abdu /Deutsche Zeitungen/
Mhariri:Abdul-Rahman