1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Rais wa Ujerumani

Abdu Said Mtullya26 Juni 2012

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya maadhimisho ya siku mia moja tokea Joachim Gauck awe Rais wa Ujerumani na pia wanatoa maoni yao juu ya mvutano uliozuka baina ya Uturuki na Syria.

https://p.dw.com/p/15LkL
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck atimiza siku 100 kazini.
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck atimiza siku 100 kaziniPicha: dapd

Kwanza maoni ya gazeti la "Braunschweiger" juu ya Rais wa Ujerumani Joachim Gauck ambaye leo anaadhimisha siku ya mia moja tokea aanze kuushika wadhifa huo. Badala ya kumpongeza, mhariri wa "Braunschweiger" anamtanabahisha Rais huyo juu ya kanuni za kidiplomasia. Anasema Rais Gauck anapaswa kuwa mwangalifu katika diplomasia ya uhusiano na nchi za nje.Mhariri huyo anaeleza kuwa Gauck anapaswa kujihadhari ili asitekeleze sera yake mwenyewe ya mambo ya nchi za nje. Mhariri huyo anasema ikiwa Rais Joachim Gauck atafanya hivyo basi atakuwa anavuka mipaka ya mamlaka yake.

Mhariri wa gazeti la "Leipziger Volkszeitung" pia anatoa maoni juu ya siku mia moja tokea Gauck awe Rais wa Ujerumani.Mhariri wa gazeti hilo anasema Gauck amekuwa Rais kwa bahati. Yumkini yeye mwenyewe aliyajua hayo siku mia moja zilizopita. Baadhi wanasiasa hawakumtaka.Pamoja na wanasiasa hao ni Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na chama cha mrengo wa shoto.Lakini katika siku hizo mia moja, Rais Gauck amerejesha imani miongoni mwa wananchi wa Ujerumani juu ya wadhifa wa Urais, kwa kutambua kwamba Rais wa hapo awali, Christian Wulff alipaswa kujiuzulu kutokana na kashfa.


Baraza la Nato limeyaitikia maombi ya Uturuki ya kuitisha kikao ili kuujadili mkasa unaohusu ndege yake ya kivita kuangushwa na Syria. Juu ya mkutano huo gazeti la "Straubinger Tagblatt" linatahadharisha: "Kutoa jibu kali juu ya mkasa wa ndege hiyo, kwa mfano kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria, kunaweza kuiingiza Urusi katika mgogoro.

Hakuna anaetaka kuliona hilo.Ni jambo la kutia moyo kwamba mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wameepuka kukaanga mbuyu.Ni kweli kwamba dilplomasia siyo jawabu lenye nguvu, lakini inawezekana ikawa hatua muhimu katika kuutenga utawala wa Assad.

Mwenyekiti wa kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu Jakob Kellenberger amemaliza muda wake. Lakini kabla ya kuondoka ameacha ujumbe mahsusi.Gazeti la "Der Neue Tag" limeandika juu ya ujumbe huo. "Tokea Marekani itoe mwito juu ya kupambana na ugaidi, sheria za kimataifa zimekuwa zinakiukwa."

Gazetzi la "Der Neue Tag" limesema Mwenyekiti wa kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu Kellenberger hakuyasema hayo wazi wazi, lakini kauli yake imebainisha wazi kwamba, haki za binadamu hazikiukwi tu, katika nchi zinazotawaliwa na madikteta, bali hayo yanatokea pia katika nchi zenye uongozi wa kidemokrasia hali inayowachochea maadui wa demokrasia.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Othman Miraji