1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yafikiria kuingia vitani Syria

17 Februari 2016

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria.Wanasema Urusi siyo mshiriki wa pekee anaeuvukuta mgogoro huo.

https://p.dw.com/p/1Hwe2
Picha: picture-alliance/dpa/Sana

Gazeti la "Der neue Tag" linasema Urusi inazidisha mashambulio ili kumpa Rais Bashar al - Assad maeneo zaidi kabla ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kuanza kutekelezwa. Lengo ni kuwasilisha ujumbe kwa nchi za magharibi kwamba si sahihi kujaribu kumwondoa Assad madarakani.

Hata hivyo, tofauti na sera ya magharibi mkakati wa Urusi na Assad haujali vifo na maangamizi yanayotokea kwa watu wa Syria.

Siyo Urusi pekee inayoukoleza moto wa Syria

Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anasema siyo Urusi pekee inayouvukuta mgogoro wa Syria kwa njia ya hatari kubwa. Bali sasa Uturuki pia inafikiria kujitosa katika mgogoro huo ndani ya nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa Uturuki inafikiria kufanya mashambulio ili kuwazuia Wakurdi wa kaskazini mwa Syria kusonga mbele.

Mhariri wa "Mannheimer Morgen" anasema Uturuki inahofia huenda sehemu hiyo ikawa mwanzo wa kuundwa nchi ya Wakurdi.

Mhariri wa gazeti la "Berliner " anasema vyombo vya habari nchini Uturuki vinaishikilia serikali yao ipeleke majeshi nchini Syria ili kuwazuia Wakurdi wanaoitwa magaidi na vyombo hivyo. Mhariri wa gazeti la "Berliner " anasema ,kwa Uturuki, mji wa Aleppo ndiyo fursa ya mwisho ya kuweza kuonyesha kuwa nchi hiyo ni muhimu, na kwamba inaweza kutoa mchango katika kuutatua mgogoro wa Syria.

Lakini mhariri huyo anaitahadharisha Uturuki kwamba mkakati huo unaweza kuwa wa hatari. Tangu mwanzo kabisa sera ya Uturuki juu ya Syria imekuwa ya maafa. Na sasa inafikiria kuchukua hatua inayoweza kulipua vita vitakavyolikumba eneo lote. Ni maoni ya mhariri wa gazeti la "Berliner" kwamba Uturuki inalekelea katika mkondo wa dafrao na Urusi nchini Syria. Ikiwa itaendelea na sera hiyo, ni wazi kwamba mgongano na Urusi hautaepukika.

Wakimbizi wa Syria kwenye mpaka wa Uturuki
Wakimbizi wa Syria kwenye mpaka wa UturukiPicha: Getty Images/C. McGrath

Gazeti la "Süddeutsche" linatathmini ushiriki wa Urusi katika mgogoro wa nchini Syria. Linasema mpaka sasa mkakati wa Rais Putin umethibiti kuwa wa mafanikio. Putin amejiingiza nchini Syria kufikia hatua ya kuwafanya Wamarekani na Umoja wa Ulaya warudi nyuma ili kuepusha mgongano wa ana kwa ana na Urusi.

Hata hivyo sasa, mgogoro wa Syria umeingia katika hatua ambapo Marekani na Urusi siyo majogoo ya pekee.Wapo wengine wanaowika vile vile.

Rais Putin amepiga hesabu zake kwa juu sana.Pana vurumai nchini Syria. Hakuna anaejua kwa uhakika iwapo ndege itakayotunguliwa katika siku zijazo itakuwa ya Urusi au ya Uturuki.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga