1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump adai ataibiwa kura

Admin.WagnerD3 Agosti 2016

Wahariri wanayatathmini madai ya Dolad Trump kwamba ataibiwa kura katika uchaguzi ujao nchini Marekani.Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya kuongezeka kwa umasikini barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1Jb7K
Donald Trump akihutubia Ashburn
Donald Trump akihutubia AshburnPicha: picture-alliance/dpa/EPA/Jim Lo Scalzo

Gazeti la "Stuttgarter" linasema Trump asingekuwa Trump bila ya kutoa kauli kama hizo. Lakini kwa kutoa madai kama hayo mgombea urais huyo anapandikiza mbegu za hatari. Nadharia hiyo ya uzushi inazidi kuifanya hali iwe mbaya nchini Marekani.

Mhariri wa gazeti la "Coburger Tageblatt" anazungumzia juu ya mvutano baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba wa wakimbizi uliofikiwa na pande hizo mbili. Mhariri huyo anasema mgogoro wa wakimbizi utaweza kushughulikiwa vizuri zaidi ikiwa mawasiliano na Uturuki yataanzishwa sasa.

Mhariri anasema litakuwa jambo la manufaa, ikiwa hatua za dhati zitachukuliwa,ili kujaribu kuwaruhusu raia wa Uturuki waingie katika nchi za Umoja wa Ulaya bila ya kuhitaji vibali. Pia anashauri kwamba ingelisaidia kuongeza msaada wa fedha kama fidia kwa Uturuki kwa kuubeba mzigo wa wakimbizi.Hatua hizo zitaiimarisha Uturuki, na hiyo itakuwa njia sahihi.

Mzingiro wa Aleppo bado wazidisha hofu


Gazeti la "Ludwigsburger" linasema watu katika mji wa Aleppo uliozingirwa wanahofia huenda majeshi ya Assad yakalipiza kisasi.

Mapigano yaendelea Aleppo
Mapigano yaendelea AleppoPicha: picture alliance/AA/A. Huseyin

Mhariri huyo anaeleza kwamba lengo la utawala wa Bashar -al Assad na washirika wake wa Urusi ni kupata ushindi wa kijeshi katika mji wa Aleppo na siyo kuwalinda raia. Anasema mazungumzo ya mjini Geneva yamekuwa kazi bure.Dunia inatazama ikiwa imeshika tama.Hiyo ni aibu kubwa.

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linazungumzia juu ya kuongozeka kwa umasikini barani Ulaya.Lakini mhariri wa gazeti hilo anaamini kwamba ziko njia zinazoweza kutumika ili kupambana na baa hilo.

Anaeleza kuwa kupambana na umasikini kunahitaji fedha.Lakini ziko njia za kuzipata fedha hizo. Sera madhubuti inahitajika ili kuhakikisha kwamba fedha za wale wanaokwepa kulipa kodi zinapatikana.Hakuna anaeweza kukana kuwapo kwa umasikini nchini Ujerumani.

Ndiyo sababu mhariri anasisitiza kwamba pana haja ya kuwazota kodi zaidi wale wenye kikubwa ,badala ya kuwapa nafuu watu hao. Hatua kama hiyo maana yake ni kutenda haki.

Mwandishi: Abdu Mtullya/ Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef