1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Wapigakura wa Afghanistan wamedanganywa

Florian Weigand/Mohammed Khelef22 Septemba 2014

Wagombea urais wa Afghanistan walisaini mgao wa madaraka kabla ya hata matokeo ya uchaguzi kutangazwa tena baada ya kura kuhesabiwa upya na Florian Weigand wa DW anasema hii ni hatari kwa demokrasia.

https://p.dw.com/p/1DGjl
Ashraf Ghani (kushoto) na Abdullah Abdullah, mahasimu wa kisiasa wanaounda serikali ya pamoja nchini Afghanistan.
Ashraf Ghani (kushoto) na Abdullah Abdullah, mahasimu wa kisiasa wanaounda serikali ya pamoja nchini Afghanistan.Picha: picture-alliance/AA

Hata kama unajuwa kwamba unapaswa kujtayarisha kwa tukio lolote nchini Afghanistan, bado nchi hii haiachi kukushangaza na vituko vyake. Nani ambaye angeliweza kufikiria kwamba baada ya mchakato wa miezi sita wenye hatua mbili za uchaguzi, ambao ulijumuisha uhisabuji kura wenye utata, mazungumzo ya simu na ziara zisizokwisha za wanasiasa kutoka ulimwengu mzima, ungemalizika kama umweso, kufumba na kufumbua? Kwamba kungelikuwa na washindi tu na hakuna aliyeondoka mtupu?

Ni jambo la kufadhaisha mno kiasi cha kwamba hata raia wenyewe wa Afghanistan wanatikisha kichwa kwa mshangao. Mitandao ya kijamii imejaa kauli mbaya dhidi ya viongozi, nyingi zao za hasira na fadhaa zinazoonesha taswira mbaya huko twendako. Lakini watu wengi zaidi wameacha hata kuzungumzia hili, pakiwa na hisia za maafa kabisa.

Miezi michache iliyopita, hali ilikuwa tafauti. Licha ya kubahatisha kupoteza maisha au viungo vya mwili, raia wa Afghanistan walijazana kwenye vituo vya kupiga kura mara mbili, mwezi Aprili na Juni, kupiga kura zao.

Dunia ikaoneshwa taswira ya matumaini, demokrasia ilikuwa nusura itiwe mkononi. Baada ya duru ya kwanza, Abdullah Abdullah alikuwa akiongoza, lakini kwenye duru ya pili ni Ashraf Ghani aliyekuwa mshindi.

Florian Weigand wa Idhaa ya Dari na Pashtun.
Florian Weigand wa Idhaa ya Dari na Pashtun.Picha: DW/P. Henriksen

Matokeo hayo yakazusha shaka, kukawa na tuhuma za wizi wa kura. Kura zikahesabiwa tena chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, wagombea hao wawili wanajaribu kuunda serikali ya pamoja. Baada ya ngia-toka nyingi, hatimaye makubaliano yakasainiwa siku ya Jumapili.

Hatari kwa demokrasia

Lakini wazo la kuwashirikisha wagombea wote wawili kwenye serikali linaonekana kama ni njia kuhalalisha uovu, na kwa demokrasia ya mashaka ambayo Afghanistan inayo, wazo hili litamalizikia kwenye hasara.

Kwa nini? Kwa sababu wapiga kura watafahamu kuwa kura zao hazina maana, kwani hatimaye wanasiasa wanaoshindania vyeo wanaweza kukaa na kuamua nani awe nani serikalini na waiongoze vipi serikali hiyo.

Kumbuka kwamba makubaliano hayo yalisainiwa hata kabla ya matokeo rasmi hayatangazwa: Ghani atakuwa rais na Abdullah atakuwa waziri mkuu mtendaji, nafasi mpya kabisa kuundwa nchini humo.

Kitu kibaya zaidi ni kuwa masaa machache baadaye, tume ya uchaguzi inamtangaza Ghani kuwa rais bila ya kutangaza takwimu zozote madhubuti au mshindi hasa. Hili kwa hakika linaonesha utovu wa adabu kwa wapiga kura na, juu ya yote, ugoigoi wa demokrasia.

Ukichukulia uzoefu wa demokrasia hii iliyoingizwa kutoka Magharibi nchini Afghanistan, halitakuwa jambo la kushangaza kama raia wa Afghanistan watakuja kuradua aina nyengine ya serikali.

Mwandishi: Florian Weigand
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman