1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vitisho vya Trump ni kinyume na maadili ya Marekani

Iddi Ssessanga
22 Desemba 2017

Majibu ya utawala wa Trump juu ya azimio la UN kuhusu hadhi ya mji wa Jerusalem yanaonyesha rais huyo yuko tayari kucheza mchezo wa wafuasi wake hata kwenye jukwaa la kimataifa, anasema Michael Knigge katika maoni yake.

https://p.dw.com/p/2pqTO
USA UN Botschafterin der USA Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley.Picha: picture alliance/dpa/AAM. Elshamy

Kwanza kabisaa tunapaswa kuweka mambo mawili wazi. Ni haki ya Rais Donald Trump kuitambua kivyake Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, hata kama hili linakwenda kinyume na sera ya muda mrefu ya Marekani ya kutoegemea upande, na hata kama hili linakiuka onyo zilizotolewa na washirika wa Marekani kutoka mataifa ya Ulaya na ya Kiarabu kutofanya hivyo.

Vivyo hivyo ni haki pia kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuelezea kutoridhishwa kwao na uamuzi wa Trump kwa kupigia kura azimio ambalo - bila kuitaja Marekani na rais wake moja kwa moja -  lilikosoa hatua yake na kusisitiza kuwa hadhi ya mwisho ya Jerusalem itaamuliwa kupitia majadiliano kulingana na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu jambo hilo.

Katika muktdha huo, ni muhimu kubainisha kwamba azimio hilo halifungamanishi, hii ikimaanisha kuwa halina nguvu ya kisheria na hivyo ni la Kiishara kwa sehemu kubwa.

Uborongaji wa utawala

Ingawa azimio hilo halina madhara yoyote ya kivitendo, utawala wa Trump ulivurunda katika kulishughulikia. Imeonyesha dhahiri namna utawala huo ulivyoonyesha kuvurunda katika jambo hili dogo la sera ya kigeni.

Hili halikupaswa kuja kama jambo la kushangaza hata kwa mtu ambaye amekuwa akifutialia kwa pembeni, mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa kipindi cha miongo miwili iliopita, kwamba hatua kama ya Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel ingepelekea mataifa ya Kiarabu na mengine kupinga uamuzi huo katika Umoja wa Mataifa.

Ukifahamu hili, na bila uwezo wa kuzuwia kile ambacho ni onyesho la kiishara la upinzani kwa hatua ambayo ni ya utata, utawala wa Trump ulipaswa tu kutoa taarifa ya kukosoa kura hiyo ikiambatana na kiapo kwamba Washington inasimamia uamuzi wake.

Lakini kama ilivyotarajiwa, utawala wa Trump ulichagua kutofanya hivyo. Badala yake iliingia  mzimamzima katika makabiliano.

Michael Knigge Kommentarbild App
Mwandishi wa DW Michael Knigge.

Wakati tabia ya rais huyo alieko madarakani kumshambulia kila anaethubutu kumpinga, kumkosoa au kumfanyia mzaha kupitia twitter imepungua kwa kiasi fulani, kumuona balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley akitumia mtandao huo kutoa vitisho kwa mataifa yanayopanga kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa kwamba Marekani itakuwa inaandika majina, ni jambo lililopotoka.

Lina sauti ya mtawala wa kibabe anaewalaazimisha walio chini yake kusalimu amri - na siyo ya mwakilishi wa nchi ambayo kijadi inajichukulia kuwa nguzo ya demokrasia.

Kinachosumbua zaidi, ambacho ni vigumu kuhukumu siku hizi, ni kitisho kwamba Marekani ingekata msaada kwa mataifa yanayounga mkono azimio hilo na barua ya onyo iliyotumwa na Haley kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa kabla ya kura hiyo.

Sauti ya utawala wa kiimla

La mwanzo si tu lingeyaumiza mataifa yalioathirika, lakini pia Marekani yenyewe, kwa vile msaada huo unaipa Marekani nguvu ya ushawishi katika mataifa hayo.

La mwisho lilifikia kilele katika sentensi inayosema "Rais atakuwa anafuatilia kura hii kwa uangalifu na ameomba niripoti kwake juu ya waliopiga kura dhidi yetu," jambo linalosikika kama mwalimu wa shule ya msingi anaewatishia wanafunzi watukutu kwamba mkuu wa shule anawafuatilia.

Ushamba wa utawala wa Trump

Hili linasikika kama kichekesho, lakini siyo kichekesho. Kwanza, kwa sababu linaonyesha kwamba hisia za utawala wa Trump na mkakati wake wa diplomasia ya kimataifa vinaweza kujumlishwa kama "njia yangu au njia kuu," ambayo ni nakala ya mkakati wa ndani uliompelekea Trump kuchaguliwa.

Pili, inaonyesha ushamba wa utawala wa Trump kuamini kwamba kuyatishia mataifa huru unaweza kuwa mkakati wa busara, ukweli unaoshadidiwa na matokeo ya kura hiyo.

Na tatu, inaonyesha utayarifu kwa upande wa utawala wa Trump kudhoofisha hata kilichobakia katika nia njema ya Washington na wahirika wengi muhimu wa kimataifa kwa ajili ya kuwaridhisha wafuasi wake wa ndani.

Mwandishi: Michael Knigge/DW Politik

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Yusuf Saumu