1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Viktor Orban anaudhihaki Umoja wa Ulaya

Mohammed Khelef
2 Aprili 2020

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amesitisha utawala wa sheria kwa kipindi kisichojulikana kwa kisingizio cha vita dhidi ya corona, lakini Bernd Riegert anasema Umoja wa Ulaya haupaswi kumnyamazia kimya.

https://p.dw.com/p/3aKuO
Ungarn Viktor Orban, Premierminister
Picha: Reuters/B. Szabo

Jibu la Kamisheni ya Umoja wa Ulaya kwa sheria za dharura za Hungary ni dhaifu na la kutia aibu. Rais wa Kamisheni hiyo, Ursula von der Leyen, alisema tu kuwa mataifa yote wanachama yanapaswa kuheshimu utawala wa sheria na kuweka mizania wakati wa kuchukuwa hatua za kukikabili kirusi cha corona, na kwamba kile kinachoendelea nchini Hungary kinafuatiliwa na kuchunguzwa kwa umakini.

Hili halitamfurahisha Viktor Orban, ambaye wabunge wanaomkosoa kwenye bunge la Ulaya, tayari wanamuita "Dikteta wa COVID." Mbabe huyo kutoka Budapest amekuwa akipambana na Brussels hata kabla ya mripuko wa corona.

Riegert Bernd Kommentarbild App
Bernd Riegert

Hata kabla ya kutolewa taarifa rasmi ya Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Orban tayari alishaukashifu Umoja huo kupitia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali, akisema kuwa endapo nchi yake haipokei msaada kwenye vita dhidi ya kirusi cha corona, basi lazima ijisaidie yenyewe. Tuhuma zenyewe si za kweli, kwani Hungary inapata msaada sawa na yapatavyo mataifa mengine wanachama.

Kirusi kinaula utawala wa sheria

Hofu za kuelemewa kwa mfumo wa huduma ya afya na mzozo wa kiuchumi kutokana na kusambaa kwa kirusi hicho havipaswi kuchukuliwa kama kisingizio cha kuufumbia macho utawala wa kidikteta wa Hungary chini ya Viktor Orban. Madaraka ya bunge kuidhibiti serikali yameondolewa kwa muda usiojulikana. Ile fursa ya mwisho ya wapinzani kutoa na kupendekeza maoni yao sasa imezuiwa. Uhuru wa kujieleza ni kama vile haupo. Hili si jambo linalokubalika kwenye demokrasia ya Ulaya na kwa uwazi kabisa linakinzana na misingi ya Mkataba ya Umoja wa Ulaya.

Kamisheni ya Ulaya, ikiwa ndiyo mlinzi wa Mkataba huo, haina njia nyengine yoyote ila kuishitaki Hungary kwenye Mahakama ya Haki ya Ulaya nchini Luxembourg. Andasa za Waziri Mkuu Orban kwamba anaweza kutumia mwanya wa vita dhidi ya corona na Umoja wa Ulaya usiweze kumshughulikia kwa kuwa umebanwa na vita hivyo kwa sasa zisiachiwe kushinda.

Hakuna mengi ya kuchaguwa

Hata kama kesi ambazo tayari ziko mahakamani hapo chini ya Kifungu cha 7 cha Mkataba wa Umoja wa Ulaya, ziko njia panda kwa mataifa mengi kusita kutekeleza hukumu zake, bado ndio njia pekee kwa sasa. Viktor Orban anaweza akajihakikishia uungwaji mkono kutoka Poland na mataifa mengine ya Ulaya Mashariki, ambayo yanapuuzia tabia yake ya kidikteta kwa maslahi yao wenyewe.

Ukweli ni kuwa hata Poland yenyewe ina kesi chini ya Kifungu hicho hicho Namba 7, kwa sababu ya kukiuka utawala wa sheria. Lakini, bado Orban anastahili kushughulikiwa, maana hujuma zake dhidi ya utawala wa sheria katika kipindi hiki cha vita dhidi ya kirusi cha corona, zitachukuliwa kuwa ni kigezo cha kufuatwa na viongozi wengine wa siasa kali za mrengo wa kulia na wafuasi wa siasa za mihemuko.