1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ujerumani ilinde misingi yake kupambana na chuki

Ines Pohl
18 Aprili 2018

Mashambulizi ya maneno yaliyoelekezwa kwa vijana waliovalia kivazi cha Kiyahudi mjini Berlin yamezusha hasira nchini Ujerumani, na mhariri mkuu wa DW, Ines Pohl, anasema sasa taifa lazima liamue kuilinda misingi yake.

https://p.dw.com/p/2wHWh
Kippa
Picha: picture-alliance/NurPhoto/A. Widak

Limekuwa jambo la kuhuzunisha linalojirejea mara kwa mara kwamba picha za vidio hujitokeza mitandaoni zikionesha kuzidi kwa chuki dhidi ya jamii ya Kiyahudi. Wakati mwengine ni bendera ya Israel ikichomwa moto, wakati mwengine mtu anayemzungumzia mmiliki wa mkahawa wa Kiyahudi juu ya mahandaki yenye gesi za sumu.

Na kila tukio moja kati ya hayo, huchochea wimbi la lawama na ukosowani. Wanasiasa huahidi kufanya kila wawezalo kuwalinda Mayahudi nchini Ujerumani. Hufanya marejeo kwenye historia na wajibu wa taifa hili, huteuwa mwakilishi, hutangaza miradi ya kielimu. 

Na huzungumzia kuhusu changamoto changamano zilizopo kwenye nchi hii, ambayo ni hivi karibuni tu imeamua kutambua rasmi kwamba hata yenyewe nayo ni taifa la wahamiaji.

Hata hivyo, vidio iliyosambaa sasa inaonesha ukatili unaothibitisha kwamba yote hayo hayatoshi kupambana na watu wasio khofu kusema wanachokiamini kama kijana huyu wa kiume anayejihisi yuko huru kumwaga hadharani chuki zake dhidi ya Mayahudi. 

Mashambulizi bila hofu?

Katikati ya mji mkuu, Berlin, kwenye uwanja wenye shughuli nyingi, mchana kweupe, kijana mwenye asili ya Kiarabu anamshambulia kijana mwenziwe aliyevalia Kippah, akishiria kuwa yeye ni Yahudi.

Mbele ya uso wake anamwaga maneno ya chuki huku akivua mkanda wake. Hakujiziba uso. Si kwamba hataki aonekane. Kinyume chake, ni kuwa huyu anajuwa kuwa anarikodiwa, maana mtu anayemshambulia ana kamera ya simu mbele yake, huku akimwambia tena na tena, kwamba anamrikodi.

Lakini ni wazi kwamba jambo hilo hata halikumshughulisha kijana huyu. Kwamba anarikodiwa, kwamba anatambuliwa na kwamba polisi hatimaye watamtia mikononi.

Kwa haya, mtu anaweza kujiuliza: Hivi hapa Ujerumani kinajiri nini siku hizi? Vidio hii ni ushahidi wa kuogofya kwamba jamii ya Kijerumani inahitaji haraka kusaka majibu ili kulinda misingi ya mtangamo wetu. Zile adhabu za kawaida zinaonekana hazifanyi ya kutosha kuwarudisha nyuma wahalifu kama hawa.

Ujerumani italinda misingi yake?

Ines Pohl Kommentarbild App
Ines Pohl, mhariri mkuu wa DWPicha: DW/P. Böll

Labda tutupie jicho kinachoendelea kwenye maskuli kuweza kutusaidia kujua tuliposimamia. Kwa miaka sasa, walimu wamekuwa wakijaribu kuitahadharisha jamii kwamba vijana wamekuwa wakitumia neno “Yahudi” kuapizana. Ukiangalia kwenye maandishi ya wanamuziki wa kufokafoka utagundua kuwa jamii ya Kijerumani inakubaliana kuwa chuki dhidi ya Mayahudi hazina nafasi kwenye taifa hili. Hakuna namna yoyote ya kujihusisha nazo na wala kuzikubali.

Litakuwa jambo lisilo sahihi kusema kwamba hivi leo Yahudi ajichukulie kuwa endapo atatembea mitaani akiwa amevaa kivazi kinachomtambulisha imani yake, basi atashambuliwa. Lakini pia itakuwa si sahihi kusema Yahudi hapaswi kuhofia kushambuliwa kwenye mitaa ya Ujerumani endapo amevaa kinachomtambulisha dini yake.

Na ni kweli kabisa kabisa kwamba njia zilizopo sasa hazifai au hazitoshi tena kuhakikisha vyenginevyo. Ujerumani imefika mahala ambapo lazima iamuwe kwa namna gani inataka kupambana waziwazi kwa maslahi ya misingi ya ustaarabu wake na pia kwa uhuru wake wa kijamii.

Mwandishi: Ines Pohl
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman