1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingiliaji wa Kanisa katika siasa Congo ni hatari

8 Januari 2019

Matokeo ya uchaguzi tayari yemecheleweshwa — Pigo jengine kwa demokrasia ya taifa hilo. Lakini shinikzo la Kanisa Katoliki linaweza kuchochea machafuko, anaandika Isaac Mugabi.

https://p.dw.com/p/3BCf3
Kongo Notre-Dame in Kinshasa
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Hatua ya kuahirisha tangazo la matokeo ya awali lililopaswa kutolewa siku ya Jumapili inatishia kuitumbukiza nchi hiyo katika machafuko ya kisiasa kutokana na uingiliaji wa Kanisa Katoliki. Kwenye mkutano wake na waandishi habari mwishoni mwa Juma lililopita, Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo lilitangaza kuwa linamjua mshindi wa uchaguzi huo -- lakini lilikataa kutaja ni nani hasa.

Katika mataifa mengine ya Afrika kama Cameroon na Uganda, Kanisa Katoliki limekuwa likichukua tahadhari katika kutoa matamko yenye mwelekeo wa kisiasa kwa kuhofia mkwaruzano na serikali. Lakini nchini Congo Kanisa lina historia ya kuingilia siasa.

Mwaka 2011, utiitifu wa Kanisa uligawika pakubwa, hivyo liliamua kutochapisha matokeo, licha ya ushahidi wa dhahiri wa kasoro na wizi wa kura ambavyo waangalizi wake walishuhudia kwene vituo vya kupigia kura.

Mambo kama hayo ni ya kufedhehesha, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba Kanisa ndiyo kimbilio la wafuasi wa upinzani hasa mjini Kinshasa katika nyakati ngumu. Wengi wana wasiwasi kwamba mteule wa Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary atashinda -- na walikuwa wanalitegemea Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Congo CENCO, lililokuwa na mtandao wa waangalizi elfu 40, kutoa matokeo ya kuaminika.

Kutokana na kuzimwa kwa mawasiliano ya intaneti kulikowaacha raia gizani, pamoja na vurugu zilizohanikiza kampeni za uchaguzi na  na wasiwasi mkubwa wa kinyang'anyiro hicho, njia iliyochukuliwa na Kanisa ni ya kizembe na hatari.

Isaac Mugab
Mwandishi wa DW Isaac MugabiPicha: DW/Abu Bakarr Jalloh

Hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kwa faragha kujadili uchaguzi huo liliamua kutotoa tamko licha ya kukutana kwa zaidi ya masaa mawili, na badala yake liliungana na mataifa mengi ya Afrika katika kuihimiza seeikali kutoa matokeo kwa amani na kuhakikisha ustahamilivu.

Ongezeko la wasiwasi

Wasiwasi umeendelea kuongezeka nchini kote, na inaonekana kwamba katika siku zijazo, Kanisa Katoliki litaendelea kuiwekea shinikizo tume ya uchaguzi kutangaza matokeo. Lakini shinikizo hili linaweza pia kusababisha maandamano na ukandamizaji dhidi ya maandamano hayo. Katika kipindi cha muda mfupi, hii inaweza kumaanisha mateso kwa mamilioni ya Wacongo ambao wamekaa kwa amani kidogo tu tangu uhuru mwaka 1960.

Badala yake, Kanisa linaweza kufanya vizuri kwa kuwajibika zaidi kupitia jukumu lake la upatanishi kati ya serikali na jamii. Desemba 2016 kwa mfano, Kanisa liliratibu makubaliano kati ya upinzani na serikali yaliomruhusu Kabila kusalia madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake hadi uchaguzi ukamilike. Tangu wakati huo hata hivyo, Kanisa limeonekana kupendelea zaidi kufanya kazi na mashirika ya kiraia na upinzani kuliko serikali.

Mashirika kama hayo huenda yakachukulia wazo la Kanisa kuwa mpatanishi kama lisilopendeza, lakini litakuwa la uwajibikaji zaidi kuliko kuchochea tu, kama lilivyofanya kwa kuchokoza matokeo ya uchaguzi kwa wapigakura ambao tayari wamehamaki.

Kusema kweli ushawishi wa Kanisa katika siasa za Congo ni mkubwa sana. Mara nyingi limejaza ombwe kwa Wacongo wengi katika taifa ambako mifumo rasmi imeshindwa kutimiza matarajio - kuanzia elimu, afya na chakula hadi kwenye maadili na msaada wa kiroho.

Ukandamizaji wa mwaka uliopita dhidi ya waandamanaji katika majengo ya Kanisa huenda ulisababisha viongozi kurudi nyuma -- lakini kuchukuwa hatua ya kijasiri sasa kushirikiana na serikali na mashirika ya kiraia kunaweza kusaidia pakubwa kutuliza wasiwasi nchini humo.

Mwandishi: Isaac Mugabi

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Caro Robi