1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Matamshi ya Rais Kenyatta yahatarisha amani Kenya

18 Juni 2014

Nchini Kenya watu zaidi ya 60 wamepoteza maisha kutokana na shambulio la bomu. Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabaab kutoka Somalia limekiri kuhusika na shambulio hilo.

https://p.dw.com/p/1CL1B
Mhariri wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt.
Mhariri wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt.Picha: DW

Pamoja na hayo rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameshutumu upande wa upinzani kuwa wanahusika na shambulio hilo. Ni hali inayotisha , kwamba amani nchini Kenya inavurugika kutokea ndani , anasema hivyo Andrea Schmidt katika maoni yake kuhusu hali nchini Kenya.

Ni kosa kubwa na propaganda ya hatari. Kundi la kigaidi la al-Shabaab limekiri kuhusika na shambulio hilo katika jimbo la pwani nchini Kenya , na serikali ya Kenya inakuja na matamshi ya hatari na kuushutumu upinzani kuwa unahusika na shambulio hilo.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametaka kuwe na mjadala wa kitaifa baada ya safari yake ya muda mrefu nchini Marekani. Ili kuutokomeza ukabila , mapambano dhidi ya ufisadi , pamoja na mabadiliko yanayodaiwa kwa muda mrefu ya vyombo vya usalama , kama ilivyoelezwa katika katiba mpya .

Serikali bado haijaliangalia hilo. Kwa kuwa upinzani unataka kutatua matatizo haya kwa ajili ya hali ya baadaye nchini Kenya, serikali inajaribu kutupa lawama kwa upinzani ili kupoteza lengo kutokana na hatua zake za kuburuza miguu.

Vyombo vya usalama nchini Kenya hushutumiwa kuwa havina uwezo, hutumia nguvu kupita kiasi na vimetapakaa rushwa. Hadi sasa haijaelezwa wazi ni nani amehusika katika kushambulio dhidi ya jumba la maduka mjini Nairobi la Westgate. Mwezi Septemba 2013 baadhi ya magaidi walivamia jengo hilo ambalo lina ulinzi mkubwa.

Katika mkasa huo watu 67 walipoteza maisha. Ni watu wangapi waliuwawa na mashambulio hayo ya al-Shabaab ama hata na wanajeshi wenyewe wa Kenya, pamoja na washambuliaji wangapi waliobakia , hilo halijawekwa wazi.

Pamoja na kitisho kikubwa kutoka kwa kundi la al-Shabaab kutaka kufanya mashambulizi mapya hakuna hatua dhabiti zilizochukuliwa kuweka ulinzi imara kwa nchi nzima. Inawezekanaje kwamba kundi la kigaidi la Wasomali liliingia nchini Kenya Jumapili iliyopita, na kwa muda wa saa nzima wakafanya unyama wa kuwauwa watu bila huruma, wakachoma moto majumba na hatimaye kutoweka bila kuonekana.

Hali hii ya kutoweza kuwalinda raia pamoja na siasa za mivutano ya ndani , zinalinufaisha zaidi kundi hili la kigaidi ambalo lina mahusiano na kundi la al-Qaeda. Kenya iliyo dhaifu ni faida kubwa kwa magaidi hao. Kuna hatari ya kuleta hali ya kuvurugika kwa amani.

Serikali inayoongozwa na muungano wa Jubelee ya rais Uhuru Kenyatta na upande wa upinzani unaoongozwa na Raila Odiga kutupiana lawama , ni jambo ambalo halina faida kabisa kwa Kenya.

Mwandishi: Andrea Schmidt / Mtafsiri: Sekione Kitojo

Mhariri: Yusuf , Saumu