1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mashaka ya AU kwa DRC yatilika mashaka

Mohammed Khelef
18 Januari 2019

Si jambo maarufu sana kwa Umoja wa Afrika kwenda kinyume na matangazo rasmi ya tume za uchaguzi za mataifa wanachama, lakini mara hii Umoja huo unayashuku matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/3Bn9J
Äthiopien AU-Gipfel in Addis Adeba
Picha: Getty Images/AFP/M. Bhuiyan

Hali ya Kongo haina tafauti sana na kile kilichowahi kutokezea kwengineko Afrika, isipokuwa tu kwa jambo moja - tume ya uchaguzi huko ilimtangaza mpinzani mmoja kumshinda mpinzani mwengine kwenye uchaguzi ambao wengi wanaamini mpinzani aliyetangazwa kushindwa ndiye mshindi halali.

Lakini si Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) wala Umoja wa Afrika uliowahi kuonesha kushughulishwa sana kwenye mataifa hayo mengine ambako aliyetangazwa siye hasa aliyeshinda.

Kwenye kesi ya Kongo, sio tu kwamba Umoja wa Afrika  umetaka kusitishwa kwa matangazo ya mwisho ya matokeo ya kura, bali pia umeamua kutuma ujumbe mzito ukiongozwa na mwenyekiti wa sasa, Rais Paul Kagame, kwenda Kinshasa kusaka mwafaka wa kisiasa baina ya pande hasimu.

SADC, kwa upande wake, sio tu imetaka kuhisabiwa upya kwa kura, bali pia imetaka baadaye paundwe serikali ya umoja wa kitaifa. Nasaha hizi nzito zinatilika mashaka.

Sababu za mashaka

DW Kiswahili | Mohammed Khelef
Mohammed Khelef, Idhaa ya KiswahiliPicha: DW/L. Richardson

Mashaka haya yana sababu kadhaa, lakini kubwa yao ni tabia isiyo ya kidemokrasia ya viongozi wengi wa Afrika, ambayo imekuwa kikwazo kwa mafanikio ya demokrasia ndani ya mataifa yao wenyewe.

Chukulia mfano wa mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye amekuwa rais kwa takribani mwaka wa 20 sasa. Rikodi yake mwenyewe ya chaguzi ni ya vituko vitupu.

Mwaka jana, alishinda kwa asilimia 99 kwenye uchaguzi ambao ulitanguliwa na mabadiliko ya katiba yaliyoondowa mihula miwili ya urais na hivyo kinadharia kumruhusu yeye kusalia madarakani hadi mwaka 2034. Mabadiliko hayo yalipitishwa kwa asilimia 98.

Kagame hayuko peke yake  linapokuja suala la tabia mbaya ya viongozi wa Afrika dhidi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Hii ndio miongoni mwa sababu mtu anasalia na maswali kadhaa juu ya vipi sasa, kwa ghafla mmoja, viongozi hawa wanaamua kulifikisha suala la uchaguzi wa Kongo kwenye hatua hii.

Mkono wa nyuma ya pazia

Inafahamika kuwa Ubelgiji, mkoloni wa zamani wa Kongo, ilionesha mashaka tangu siku ya kwanza ya matangazo ya uchaguzi. Mashaka yameoneshwa pia na Ufaransa na Marekani. Je, inawezekana kuwa nyuma ya pazia, viongozi wa Umoja wa Afrika wameshajiishwa kuwa na msimamo huu na mataifa haya makubwa?

Ingawa sipingani na kuwaona viongozi wa Kiafrika wakiongoza jitihada za kusaka suluhisho kwa matatizo ya Afrika, mashaka yangu hasa yapo kwenye chimbuko la hilo suluhisho lenyewe.

Amani na utulivu zinapaswa kuwa shabaha ya juhudi hizo, lakini wakati huo huo, viongozi hawa hawapaswi kusahau misingi ambayo demokrasia imejengewa, nayo ni uhuru, haki za binaadamu na ushiriki wa wananchi.

Ule wakati wa timu za waangalizi wa Umoja wa Afrika kuelemea upande wa tume za uchaguzi umepita.

Mwaka 2017, waangalizi hao waliuunga mkono uchaguzi wa Kenya ambao baadaye ulikuja kufutwa na Mahakama ya Juu kwa kukiuka kwake katiba. Waangalizi hao pia hawakulalamika kwenye chaguzi za Gabon, Zambia, Chad wala Uganda, ambazo ndani ya miaka mitatu iliyopita zilikuwa mfano wa chaguzi zisizo na uwazi wala haki.

Zama hizo zinapaswa sasa zikome!

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf