1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Juhudi zaidi zahitajika kukabiliana na chuki dhidi ya Wayahudi

Admin.WagnerD15 Septemba 2014

Viongozi wote wa kisiasa wa Ujerumani walijumuika mjini Berlin kupinga chuki dhidi ya Wayahudi wakiungana na watu weingine 6000, lakini hiyo haitoshi kabisaa, anasema Mhariri mkuu wa Deutsche Welle Alexander Kudaschef.

https://p.dw.com/p/1DCMr
Demonstration gegen Antisemitismus in Berlin 14.09.2014
Picha: Reuters/Bernd von Jutrczenka

Ni ishara ya wazi - watu 6000 wamekusanyika mjini Berlin kupinga chuki dhidi ya Wayahudi. Ni watu 6000 tu na siyo zaidi. Mwaka 1992, zaidi ya Wajerumani milioni moja walifanya mihadhara ya kuwasha mishumaa mijini na vijijini nchini kote kupinga ubaguzi wa rangi. Huo ulikuwa wakati ambapo chuki ya makundi ya itikadi kali za mrengo wa kulia ilikabiliwa kwa nguvu ya maandamano.

Lakini mara hii, watu 6000 ndiyo wamezungumza. Idadi hiyo inahusisha viongozi wote wa serikali ya Ujerumani - Rais, Kansela, Mawaziri, watetezi wa muungano, makanisa ya Kiprotestant na Kikatoliki. Wote walikusanyika Jumapili kutoa tamko la wazi kupinga chuki dhidi ya Wayahudi - kwa mwaliko wa baraza kuu la Wayahudi nchini Ujerumani, kwa sababu hakuna juhudi zilizofanywa na jamii kutoka ndani ya Ujerumani yenyewe. Hilo ni jambo la fedheha, kama ilivyo idadi ndogo ya washiriki.

Mhariri mkuu wa Deutsche Welle Alexander Kudascheff.
Mhariri mkuu wa Deutsche Welle Alexander Kudascheff.Picha: DW/M. Müller

Ni ukweli usiyopingika kwamba kuna upungufu katika namna Wayahudi wanavyochukuliwa, hasa kutokana na vile watu wanavyoiona Israel. Umma wa Wajerumani umeanza kuikosoa Israel zaidi kuliko unavyoikosa serikali. Na nyuma ya mtizamo huu wa kuikosoa Israel, kuna chuki zinazojitokeza dhidi ya Wayahudi, zinazoonyeshwa mitaani na wahamiaji Waislamu, zinazosambazwa kwenye mitandao na Wajerumani wa kawaida.

Kiwango cha matamshi machafu, chuki na hasira dhidi ya Wayahudi kinachokutikana si tu kinadhalilisha na kufedhehesha, lakini pia kinasumbua akili. Na ndiyo sababu mkutano uliyofanyika mjini Berlin kwenye lango la Brandenburg ndiyo lilikuwa tamko sahihi: Ujerumani inahusika na mauaji ya Wayahudi maarufu kama Holocaust, yaliyogharimu maisha ya Wayahudi milioni sita wa Ulaya.

Nchini Ujerumani kunapaswa kuwa na dhamira zaidi ya kuzungumza kwa sauti na kwa msisitizo dhidi ya chuki kwa Wayahudi kuliko kwingineko. Hatuwezi kujifanya kama vile kila kitu kiko sawa. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, karibu asilimia 20 ya raia nchini Ujerumani wana mtazamo wa chuki au wanakubaliana na matamshi ya chuki dhidi ya Wayahudi. Kwa bahati mbaya chuki hiyo ni zaidi ya ilivyokuwa miaka 25 nyuma.

Miongoni mwa watu hao wamo wanaolemea mrengo wa kulia, mrengo wa kushoto, wahamiaji Waislamu na watu kutoka jamii kubwa za Ujerumani. Miaka 75 baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, baada ya mauaji ya Wayahudi, masinagogi yanalazimika kulindwa na polisi, hata shule za watoto wadogo. Wayahudi wanaovaa kofia wanashambuliwa kwa maneno. Makaburi yanachimbuliwa. Hii ndiyo hali halisi ya Wayahudi wanaoishi Ujerumani.

Lakini: Licha ya mauaji ya Holocaust, na chuki ya kila siku, wayahudi wanaendelea na maisha yao nchini Ujerumani. Kamati zinakuwa, Wayahudi hawajifichi, wanajiamini. Hilo lilikuwa bayana mjini Berlin. Wanaonyesha hisia zao. Hawatakubali fedheha na matusi. Na ndiyo maana, kama alivyobainisha Kansela, mapambano dhidi ya chuki kwa Wayahudi ni jambo la kitaifa. Jamii huru haikubaliani na chuki dhidi ya Wayahudi, na inachukia ubaguzi.

Mwandishi: Alexander Kudaschef
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Oummilkheir Hamidou