1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ishara ya kashfa ya Watergate

Admin.WagnerD10 Mei 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amemfukuza kazi mkuu wa idara ya upelelezi nchini humo, FBI, James Comey, kutokana na alivyoendesha uchunguzi wake katika kashfa ya barua pepe za Hillary Clinton.

https://p.dw.com/p/2ckxT
Washington Senat Aussage FBI Director James Comey
Picha: Reuters/K. Lamarque

Kwa kumfukuza kazi mkuu wa idara ya upelelezi ya Marekani, FBI, James Comey, Trump huenda ameanzisha tetemeko katika ulingo wa siasa, anasema mwandishi wa DW mjini Washington, Marekani, Miodrag Soric, katika maoni yake.

Hakujawahi kutokea kitu kama hiki katika historia ya Marekani. Mkuu wa ikulu ya Marekani amemfuta kazi mkuu wa idara ya upelelezi FBI katika wakati ambapo anaongoza uchunguzi ambao unaweza kugeuka kuwa hatari kwa rais. James Comey amekuwa akichunguza jitihada za Urusi kushawishi matokeo ya uchaguzi wa Marekani, lengo kubwa likiwa kumsafishia njia Donald Trump kuingia ikulu na kumhujumu mpinzani wake, Hillary Clinton.

Katika wiki chache zilizopita utawala wa Trump umeyapinga na kuyakataa madai yote kwamba ulishirikiana na utawala wa Urusi, Kremlin, wakati wa kampeni za uchaguzi 2016 na uchunguzi wa FBI ulikuwa bado unaendelea. Kumfuta kazi mkuu wa FBI kabla uchunguzi kukamilika kunasababisha mazingira mabaya na ya uchungu kisiasa kama shubiri. Sio tu wanasiasa wa chama cha Democratic wenye hofu kuhusu uwezekano wa rais Donald Trump kumteua mkuu mpya wa FBI atakayeukamilisha haraka uchunguzi huo. Hii pia itafikisha mwisho juhudi za kutafuta ukweli kamili kuhusu ushawishi wa kisiasa uliofanywa na utawala wa mjini Moscow.

Rais wa Marekani mashakani

Uamuzi wa Trump umevuruga uaminifu wa taasisi za kisiasa mjini Washington. Sifa za tabaka la kisiasa zitashuka kufikia kiwango kipya cha chini na patakuwa na ongezeko la hali ya kukata tamaa na kuvunjika moyo kisiasa. Rais anataka idara ya upelelezi FBI iwe na mwanzo mpya. Sababu ya Trump ya kumtimua Comey ni mwenendo wake kuhusiana na kashfa ya barua pepe iliyomkabili Hillary Clinton.

Soric Miodrag Kommentarbild App
Miodrag Soric, Mwandishi wa DW mjini Washington

Lakini hakuna anayeikubali sababu hiyo, hata wanachama wa chama chake cha Republican. Pamoja na hayo, si mwingine bali Trump mwenyewe aliyeusifu mwenendo wa Comey kuhusu suala hilo - baada ya uchunguzi huo kuiathiri kwa kiwango kikubwa kampeni ya mpinzani wake katika dakika za lala salama kabla uchaguzi wa Novemba 8 mwaka uliopita.  Mungu aepushe mbali isije kudhihirika miezi michache baadaye kwamba pengine palikuwa na sababu za chinichini za kufutwa kazi mkuu huyo wa FBI.

Kulazimishwa kwa Comey ajiuzulu kunaweza kusababisha tsunami ya kisiasa mjini Washington. Uamuzi huo unakumbusha kashfa ya Watergate. Ilikua mapema miaka ya 1970 wakati rais wa Marekani waakti huo Richard Nixon alipomtimua afisa maalumu wa uchunguzi ambaye alikuwa amepata taarifa kuhusu mpango wake mbaya. Haikusaidia: Nixon alilazimika kujiuzulu. Hakuweza kuizuia siri kufichuka na ukweli hatimaye kujulikana.

Trump pengine anaweza kumtimua Comey, lakini wanasiasa wa chama cha Democratic na baadhi ya wanasiasa wa chama cha Republican - wataendelea kujaribu kuchunguza kama kampeni ya Trump ilifanya mashauriano na wajumbe wa Urusi. Kufikia sasa hakuna ushahidi wowote, lakini mambo yanaweza yakabadilika.

Mwandishi:Soric, Miodrag

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Iddi Sessanga