1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malkia Elizabeth kuwasilisha mpango wa serikali bungeni

Yusra Buwayhid
21 Juni 2017

Mpango wa serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May utazinduliwa leo bungeni na Malkia Elizabeth II, baada ya chama chake kupoteza viti bungeni, pamoja na taifa hilo kutikiswa na matokeo ya maafa.

https://p.dw.com/p/2f5JG
Königin Elizabeth II. London Grenfell Tower
Picha: Getty Images/AFP/D.Leal-Olivas

Malkia wa Uingereza Elizabeth II anatarajiwa kuiwasilisha sera hiyo kwa wabunge ambao baadae wataijadili kwa siku kadhaa kabla ya kuipigia kura, huku taifa hilo likijiandaa kuanza mazungumzo ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya - mchakato unaojulikana kama Brexit. 

Malkia Elizabetha atatoa hotuba yake hiyo katika ufunguzi wa bunge kabla ya kuanza mijadala katika bunge la Uingereza (House of Commons) pamoja na katika Baraza la juu la Bunge la Uingereza (House of Lords).

Ni hotuba inayotarajiwa kuanzisha kile kinachoitwa "Mswada Mkubwa wa Kisheria wa Ubatilishaji" ambao utaruhusu kujumuisha baadhi ya sheria za Umoja wa Ulaya katika sheria za Uingereza, baada ya taifa hilo kuchana na Umoja huo kupitia mchakato unaojulikana kama Brexit.

Chama cha Conservative kimegawanyika

Chama cha Conservative hata hivyo kimegawanyika katika suala la mazungumzo ya Brexit. Kuna baadhi ya wanachama ambao ni wapinzani wa muda mrefu wa uanachama wa Umoja wa Ulaya, wanaodai kuwepo kwa mazungumzo yenye masharti mazito. Wengine, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Fedha Philip Hammond, wanadai mazungumzo yenye masharti mepesi ambayo ni pamoja na kukubali usafiri huria wa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya, na kuendelea kutambua Mahakama ya Haki ya Ulaya.

London Theresa May nach Treffen mit  DUP Leader Arlene Foster
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/J. Taylor

Baada ya kutokea mashambulizi manne ya kigaidi na jengo moja la ghorofa 24 la Grenfell Tower kuwaka moto mjini London na kusababisha hali ya majonzi nchini humo, baadhi ya raia wanapanga kuandamana katika mitaa kadhaa dhidi ya chama cha Conservative cha May katika kile walichokiita "Siku ya Hasira."

May aliitisha uchaguzi wa mapema Juni 8 akiwa na lengo la kukiongezea mamlaka chama chake bungeni, huku Uingereza ikiwa inaelekea katika majadiliano ya Brexit na Umoja wa Ulaya.

Lakini mpango wake huo ulishindikana na kukiacha chama chake cha kihafidhina  na uchache wa viti bungeni, na hivi sasa kinahitaji msaada wa chama cha kihafidhina cha Ireland Kaskazini cha DUP.

May amekataa wito wa kujiuzulu na anatumaini kupata msaada ya chama cha DUP wa viti 10 ili aongezee viti 317 ilivyopata chama chake katika uchaguzi uliopita. May anahitaji kuwa na viti 326 ili aweze kuwa na serikali ya wingi katika bunge lenye jumla ya viti 650.

Mwandishi Yusra Buwayhid/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman