1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malkia wa Katwe: Chesi ilivyobadili maisha ya Phiona Mutesi

Iddi Ssessanga
18 Januari 2018

Phiona Mutesi alijinasua kutoka katika dimbwi la umaskini kwa kucheza mchezo wa chesi. Kiliandikwa kitabu juu yake na filamu ikaigizwa kumhusu. Mwaka mmoja baadae, anaiambia DW namna chesi ilivyobadili maisha yake.

https://p.dw.com/p/2r4Gb
Uganda Schachschule Phiona Mutesi
Picha: DW/P. Shabani

Katwe ni miongoni mwa makazi makubwa duni katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.  Umaskini na mafuriko ya mara kwa mara yamefanya maisha yawe magumu kwa maelfu ya wakaazi wa eneo hilo.  Kadhalika kuondoka katika makazi hayo ni vigumu zaidi. Lakini Phiona Mutesi mwenye umri wa miaka 21 alibaini njia isiyo ya kawaida ya kutoka mitaani, licha ya kuwa, Katwe ulikuwa ni ulimwengu pekee alioufahamu.

"Unapokosa makazi na hakuna anayekujua wala hakuna anayetarajia chochote kutoka kwako na hutarajii chochote kutoka kwako mwenyewe. Niliijua Katwe tu. Hakuna aliyenihamasisha. Niliifahamu Katwe na makazi duni," aliiambia DW.

Kwa msichana ambaye alipoteza tumaini kabisa, Phiona ametoka mbali. Kama mtoto ambaye hakupata fursa ya kwenda shule na sasa ni mwanafunzi wa chuo  huko Seattle. Na amekuwa mtu ambaye hakuna aliyedhani kama atakuwepo mtu wa kuandaa filamu kuhusu maisha yake. Na msingi wa hadithi yake ya kipekee ni mchezo wa chesi au mchezo wa bao.

Mchezo wa mbinu

Ilikuwa  katika darasa la chesi linaloongozwa na kocha Robert  Katende, ambako Phiona na watoto wengine wengi kama yeye wamejifunza kitu ambacho wanakitumia katika maisha yao yote. Katende anauita ´mchezo wa mbinu.´ "Falsafa yake ni rahisi. Chesi ina mengi ya kutoa. Ni zaidi ya kushinda medali na kuwa bingwa," anasema Katende.

Uganda Schachschule Phiona Mutesi und Robert Katende
Phiona Mutesi katika shule ya mchezo wa chesi na mwalimu wake Robert Katende.Picha: DW/P. Shabani

Katende anasimamia miradi mbalimbali kwa watoto wenye uwezo. Miaka 15 iliyopita alianzisha darasa huko Katwe, ambalo liliwavutia watoto kwa kutoa chakula cha bure.

"Binafsi naangalia suala hilo kama  silaha muhimu ya uwezeshaji. Unamuwezesha mtu kupata ujuzi ambao unamsaidia maishani.  Ni mchezo wa mkakati, mchezo wa kufanya maamuzi, kutatua matatizo na kuthibiti muda. Hivyo kama unaweza kutumia ujuzi  kwenye ubao wa chesi, hautafeli maishani.

Darasa lake lina watoto wengi waliozunguka ubao wa chesi, wakicheza michezo, kwa malengo ya kina. Kijana mmoja, anafafanua kwanini waliamua kucheza bao. Anasema anacheza chesi kwa sababu inakufanya kufikiria kwa upanda zaidi. Anasema anatarajia kusimamia wanamuziki atakapokuwa mkubwa.

Safari ilivyoanza

Awali, Phiona hakuvutiwa na masomo ya chesi. Alikuwa ametingwa na kazi lakini kaka yake mkubwa alikuwa ameshajisajili katika program ya Katende ya mchezo wa chesi.

Siku moja, hamu ya kula bure ilimuingia na akamfuata kaka yake. Lakini siku hiyo alifanya mengi zaidi ya kujaza tumbo lake, alibaini kuwa ana kipaji katika mchezo huo. Ikatokea kuwa hicho kilikuwa kipindi kilichobadili maisha yake.

Mwaka 2016, filamu kuhusu maisha ya Phiona, ilitolewa, iliandaliwa na Disney na kupewa jina la Malkia wa Katwe. Kama filamu inavyojieleza, Phiona alianza kushiriki mashindano ya chesi na kupata ufadhili wa masomo.

Phiona ni hadithi pekee ya mafanikio katika programu ya chesi inayosimamiwa na Katende. Lakini  mwandishi wa habari za michezo wa Marekani,  Tim Crothers, alimchagua Phiona kama muhusika mkuu katika kitabu chake alichokipa jina Malkia wa Katwe. Baadaye kitabu hicho kilizaa filamu ya Disney.

Uganda Schachschule Robert Katende
Robert Katende akiwapa maelekezo wanafunzi wenye ulemavu tofauti katika shule ya chesi.Picha: DW/P. Shabani

Mwaka mmoja baadae

Mwaka mmoja baada ya  maisha yake kuonyeshwa katika filamu. Phiona anaeleza jinsi mchezo wa chesi ulivyobadili maisha yake.

"Chesi imenifundisha mambo mengi. Ukiangalia ubao, ni kama maisha yenyewe, unaangalia unapoanza mchezo, wakati wote unatakiwa kupanga kila kitu unachoanza. Hata katika maisha yako ya kila siku unatakiwa kupanga na kuweka mkakati. Wakati wote kuna ndoto ya kuifanikisha, hivyo unatakiwa kupanga kwa vipande ulivyo navyo ili kufikia malengo uliyo nayo,”

Leo hii, Katende, ana shule nyingi za mchezo wa chesi Uagnda, na ana wanafunzi  zaidi ya 1500. Kwake, filamu hiyo ni utambulisho mkubwa wa kazi yake na kwa watoto wote katika programu zake.

Hakika, maisha halisi si kama hadithi. Filamu hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa Phiona, Robert Katende na Katwe kwenyewe.

Kila mmoja anaweza kumsaidia mmoja

Si kwamba changamoto zao zote zimetatuliwa. Filamu hiyo haikufanikiwa sana. Phiona bado anahitaji fedha ili aendelee na chuo. Ingawa Katende amejenga madarasa mengi ya chesi, lakini idadi ya watoto imeongezeka na anakosa pa kuwaweka.

Lakini bado Phiona na Katende, hawajutii filamu hiyo kuhusu maisha yao. Katende anadhani filamu ya Malkia wa Katwe inaonyesha kuwa wakati huwezi kumsaidia kila mmoja,  kila mmoja anaweza kumsaidia mmoja.

Phiona anaamini filamu hiyo, inawahamasisha watoto duniani kote na kusaidia kudumisha matarajio yao kama ambavyo mchezo wa chesi ulivyompa kitu cha kupanda na namna ya kuandaa maisha yake.

 Mwandishi: Florence Majani/DW

Mhariri: Saumu Yusuf