1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yaomba msaada wa dharura kuzuia waasi

11 Januari 2013

Rais wa Mali ameomba msaada wa kimataifa, baada ya waasi wa Kiislamu wanaodhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kuuteka mji muhimu na kutishia kusonga mbele kuelekea kusini.

https://p.dw.com/p/17HnZ
Wapiganaji wa Ansar Dine.
Wapiganaji wa Ansar Dine.Picha: Reuters

Wakati baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likikutana katika kikao cha dharura mjini New York kujadili mgogoro huo, watu walioshuhudia wamesema zana za kivita na wanajeshi wa kigeni wameanza kuwasili kwa ndege kuimarisha majeshi ya serikali katikati mwa Mali.

Wakimbizi wa ndani wakiwasili mjini Bamako wakitokea Timbuktu, kaskazini mwa Mali.pixel
Wakimbizi wa ndani wakiwasili mjini Bamako wakitokea Timbuktu, kaskazini mwa Mali.Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa wataka kupelekwa kikosi haraka

Kufuatia kikao hicho cha dharura, Umoja wa Mataifa uliamrisha kupelekwa haraka kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Umoja wa Afrika kuzuia waasi hao, lakini mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa alisema rais wa muda wa Mali Dioncounda Traore alikuwa ametuma maombi mahususi ya msaada wa kijeshi kutoka kwa Ufaransa, mtawala wa zamani wa taifa hilo.

Taarifa ya kikao hicho ilisomwa na balozi wa ufaransa katika Umoja wa mataifa, Gerard Araud: "Azimio hili linayaomba mataifa yote wanachama, kutoa msaada wa kutatua mgogoro wa Mali, ukiwemo wa kijeshi na kisiasa, na nasisitiza, kutoa msaada kwa mamlaka ya nchi hii kukomesha kitisho cha ugaidi. Tukio hili linaonyesha tena umuhimu wa kupelekwa kwa jeshi la Umoja wa Afrika kaskazini mwa Mali, na tume ya mafunzo ya Umoja wa Ulaya."

Balozi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud
Balozi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard AraudPicha: picture-alliance/dpa

Ansar Dine watishia kusonga mbele kusini

Mapema Alhamisi, Abdou Darda kutoka kundi la Ansar Dine, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa wapiganaji wa Kiislamu walikuwa wameuteka mji wa Konna, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Mopti, ambapo walioshuhudia walisema wanajeshi wa serikali walikuwa wakirudi nyuma. Darda alisema kwa njia ya simu kuwa wanadhibiti karibu mji wote wa Konna na kuongeza kuwa walikuwa wanapanga kusonga mbele kusini. Mashahidi walisema wanajeshi walikuwa wanarudi nyuma kuelekea Sevare, karibu na Mopti. Ni katika kituo cha kijeshi cha Sevare, umbali wa kilomita 60 kutoka Konna, ambako walioshuhudia waliona ndege za kijeshi zikishusha silaha na wanajeshi wa kigeni.

Afisa wa serikali ya Mali, akithibitisha kuwasili kwa ndege hizo za kijeshi, alisema zilihusisha ndege moja kutoka nchi ya Ulaya, ambayo iliacha wanajeshi na zana katika kambi ya Sevare. Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa mjini New York  wamesema rais Traore alimuandikia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na rais Francois Hollande. Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, alisema Ufaransa itatoa msimamo wake leo, lakini alielezea hofu ya nchi yake juu ya hali ya usalama inayozidi kuporomoka.

Rais wa muda wa Mali, Dioncounda Traore
Rais wa muda wa Mali, Dioncounda TraorePicha: AFP/Getty Images

Mashaka juu ya uwezo wa jeshi la Mali

Kuanguka kwa mji wa Konna ni pigo jingine kwa juhudi za kuwazuia waasi hao wa Kiislamu. Mpaka sasa walikuwa wamebakia kaskazini walikochukuwa udhibiti miezi tisa iliyopita, na ambako mataifa ya magharibi yanahofia wanaweza kupafanya mahala salama kwa magaidi. Wanadiplomasia walisema karibu wapiganaji 1,200 wako umbali wa kilomita 20 kutoka mji wa Mopti, ambao ni njia kati ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi na yale yaliyoko chini ya serikali.

Lakini maafisa wa Umoja wa mataifa wameonya kuwa haitawezekana kupeleka wanajeshi kabla ya mwezi Septemba. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice, alisema mashaka yalionyeshwa katika kikao hicho cha dharura, kuhusu uwezo wa jeshi la Mali.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFPE
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.