1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya muda mrefu ya amani kati ya Israel na Hamas yanukia

Saumu Mwasimba13 Februari 2009

-

https://p.dw.com/p/GtJx
''Miongoni mwa mipaka inayotakiwa kufunguliwa ni pamoja na mpaka wa misri wa Rafah''Picha: AP

Jeshi la Israel limefahamisha kwamba wanamgambo wa Hamas wamevurumisha roketi tatu karibu na mji wa Sderot nchini Iraeli mapema hii leo lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Hujuma hizo zimetokea huku makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha vita yakisubiriwa kutangazwa kufuatia juhudi za kidiplomasia zilizoongozwa na Misri.

Shirika rasmi la habari la Misri limetoa ripoti kwamba naibu kiongozi wa kundi la Hamas amesema kundi hilo limekubali kusitisha mapigano na Israel kwa kipindi kirefu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza.

Mazungumzo ya kutafuta muafaka huo kati ya Israeli na Hamas yamekuwa yakisimamiwa na Misri ambayo inatarajiwa kutangaza makubaliano hayo ya amani yatakayodumu miezi 18.

Misri inatazamiwa kutangaza hatua hiyo katika kipindi cha siku mbili baada ya kushaurina na makundi mengine ya wapalestina.

Hata hivyo mjini Jerusalem ofisi ya waziri mkuu Ehud Olmert imesema serikali ya Israel haiwezi kuzungumzia kuhusu ripoti hizo.

Hapo awali maafisa wa Misri na kundi la Hamas walizungumzia juu ya kupigwa hatua katika mazungumzo hayo ya kusaka amani yaliyowakutanisha kiongozi mwenye usemi mkubwa ndani ya kundi la Hamas kutoka Gaza,Mahmoud Zahar pamoja na mjumbe wa ngazi ya juu wa Misri ambaye ni mkuu wa upepelezi Omar Suleiman.

Afisa wa ngazi ya juu wa Misri ambaye anahusika katika juhudi hizo za kutafuta amani mashariki ya Kati Moussa Abu Marzouk ameliambia shirika la habari la Misri Mena kwamba makubaliano ya amani yaliyofikiwa yanatoa mwito kwa Israel kufungua tena mipaka sita ya kuingia Ukanda wa Gaza.

Aidha duru kutoka katika mazungumzo hayo zimesema kwamba pamoja na kufunguliwa mipaka kutakuwa pia na ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza na kuitaka Israel iondoe vizuizi vyake katika eneo hilo.

Kwa upande mwingine msemaji wa Hamas ametoa taarifa ya maandishi akisema makubaliano hayo kati ya Israel na Hamas yatatangazwa rasmi katika muda wa siku tatu zijazo baada ya Hamas kutoa jibu lake la mwisho hapo jana juu ya mpango huo.

Misri imekuwa ikifanya mazungumzo na pande zote mbili katika wakati tofauti kwa lengo la kutafuta makubaliano ya amani ya kudumu ambayo yatachukua nafasi ya maafikiano dhaifu ya utulivu yaliyochangia kumalizika opresheni ya kijeshi ya Israeli ya siku 22 iliyosababisha uharibifu mkubwa katika Gaza mnamo mwezi wa Januari.

Mbali na kusimamia mazungumzo hayo ya kuleta amani Misri pia inajaribu kutafuta hali ya maridhiano kati ya kundi la Hamas na chama cha rais Mahmoud Abbas cha Fatah ili kufikia hatua ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayoendelea kuwa na mazungumzo ya amani na taifa la Israel.