1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani ya Ougadougou

Oummilkheir6 Machi 2007

Ufaransa yasaka upenu wa kujitoa katika kizungumkuti ilichojitakia wenyewe

https://p.dw.com/p/CHIq
Bendera ya Ivory Coast
Bendera ya Ivory Coast

Makubaliano ya jumapili iliyopita kati ya serikali ya Ivory Coast na waasi,ni fursa ya kujitoa kimaso maso Ufaransa-iliyotangaza papo hapo iko tayari kuachana na jukumu lake la kijeshi baada ya miaka mine na nusu katika koloni lake hilo la zamani.

Hata wino wa makubaliano hayo kati ya rais Laurent Gbagbo na mkuu wa waasi wa Forces Nouvelles-FN,Guillaume Soro,haujawahi kukauka mjini Ougadougou,waziri wa ushirikiano wa serikali kuu ya Ufaransa Brigitte Girardin ametangaza uwezekano wa kuondoka hatua baada ya hatua vikosi vya jumuia ya kimataifa.

Bibi Girardin ameitaja hali ya mambo kua ni ya “ushindi” kwa jumuia ya kimataifa na kwa Ufaransa inayotaraji chaguzi huru zitaweza kuitishwa hjadi mwaka huu utakapomalizika.

Makubaliano hayo yanazungumzia,miongoni mwa mengineyo juu ya kuundwa serikali mpya na kuondolewa,haraka wanajeshi 7800 wa tume ya Umoja wa mataifa ya kulinda amani pamoja na wanajeshi 3500 wa kikosi cha Ufaransa –Licorne,kilichopewa jukumu na Umoja wa mataifa kuepusha mapigano yasiripuke upya kati ya kambi mbili zinazohasimiana.

“Jipya ni kwamba makubaliano haya yamefikiwa na mahasimu wawili peke yao.Ni jambo lililokua likisubiriwa tangu muda mrefu uliopita-kuwaona wananchi wa Ivory Coast wakijitwalia wenyewe mustakbal wa nchi yao.” Amesema hayo waziri wa ushirikiano wa Ufaransa,Brigitte Girardin kupitia shirika la habari la Ufaransa AFP.

“Masharti ya mwanzo yameshapatikana kuwawezesha wanajeshi wa kimataifa waanze kuondoka kidogo kidogo”ameongeza kusema mwanasiasa huyo.

Hakuna ratiba iliyotangazwa lakini mjini Paris lini vikosi vya Ufaransa vitaanza kuihama nchi hiyo ya Afrika Magharibi.Waziri wa ulinzi Michele Alliot-Marie amesema mpango wa kuwahamisha wanajeshi wao unahitaji muda kuandaliwa-pengine wiki kadhaa zijazo.”

Muda wa shughuli za tume ya umoja wa mataifa nchini Ivory Coast ulikua umalizike mwishoni mwa mwezi June ujao-tareje ambayo baraza la usalama lilikua likutane kujadili kama kuna haja ya kurefushwa muda wa shughuli hizo.

Jibu la haraka la Paris linaashiria pupa ya Ufaransa ya kujipatia upenu wa kujitoa katika kizungumkuti cha kujitakia”amefafanua Gilles Yabi, ambae ni mdadisi wa shirika la International Crisis Groupe-ICG mjini Dakar-Senegal.

Vikosi vya Licorne vinaongoza shughuli kubwa kabisa za kijeshi za Ufaransa nchi za nje na vina gharimu fedha nyingi pia-yuro milioni 250 kwa mwaka,katika wakati ambapo wanajeshi wa Ufaransa wanawajibika kwengineko pia ulimwenguni-mfano Libnan.

Zaidi ya hayo, wanajeshi wa Ufaransa wanaotumikia shughuli za Licorne wamekua wakielezea hamu ya kutaka kuihama nchi hiyo,hasa baada ya machafuko ya mwaka 2004 yaliyopelekea wenzao tisaa kuuliwa na wanaanga wa jeshi la Ivory Coast.

Kutumwa wanajeshi wa Ufaransa mwaka 2002 nchini Ivory Coast kuliwazuwia waasi wasiuvamie mji wa Abidjan.Lakini Ufaransa ilishindwa pia kuwalazimisha mahasimu wawili waukubali mpango wa amani.

“Ufaransa haikua na hila mbele ya Gbagbno aliyekula kiapo kattu hatokubali kung’olewa madarakani”” amesema Gilles Yabi.

Kwa maoni ya Richard Banégas,mkuu wa jarida la “Politique Africaine” makubaliano ya Ouagadougou “yanamaanisha kushindwa Ufaransa kulazimisha njia yake wenyewe ya kujitoa katika mzozo wa Ivory Coast.-Laurent Gbagbo ndie aliyeibuka na ushindi”.

Hata hivyo Gilles Yabi anakiri hata hivyo juhudi za Ufaransa ndizo zilizoipelekea kuepusha balaa la vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast.