1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani Gaza yamalizika

Saumu Mwasimba19 Desemba 2008

Hali ya wasiwasi ndani na nje ya Gaza baada ya Hamas kukataa kurefusha muda wa amani

https://p.dw.com/p/GJb9
Hamas waliliteka eneo la Ukanda wa Gaza tarehe 14 Juni 2007Picha: AP

Ghasia zimeibuka tena katika eneo la mpaka wa Gaza na Israel baada ya makubaliano ya kusitisha vita kumalizika muda wake hii leo.

Jeshi la Israel limefahamisha kwamba wanamgambo kutoka Gaza wamevurumisha roketi mbili mapema leo asubuhi katika ardhi ya Israel.

Aidha wanajeshi wanaowalinda wakulima wakiisraeli katika eneo hilo la mpakani wamakabiliwa na mashambulio makali kutoka Gaza.Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa kufuatia mashambulio hayo.Mapema hii leo kundi la Hamas lilitangaza kwamba makubaliano hayo ya miezi sita ya kusitisha vita yamemalizika na hayataongezewa muda.

Msemaji wa kundi la Hamas linalodhibiti mamlaka katika ukanda wa Gaza Fawzi Barhoum alisema tangu jana kwamba hakuna uwezekano wa kuongezewa muda kwa makubaliano hayo ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Misri mwezi wa Juni.Tawi la Hamas la al Qassam Brigade limesema kwamba sababu kubwa inayowafanya kuendelea na harakati za ghasia dhidi ya Israeli ni kutokana na Israeli kushindwa kuondoa vizuizi vyake katika ukanda wa Gaza na pia ilikataa makubaliano hayo ya kusitisha vita yatekelezwe hadi ukingo wa magharibi.

Katika taarifa yake kundi hilo limeapa kuilinda ardhi ya wapalestina na kuwakomboa wapalestina huku wakiionya Israeli dhidi ya kuanzisha tena utumiaji wa nguvu.Hali hiyo imezusha wasiwasi mkubwa katika eneo zima la mashariki ya kati na kwa jamii ya kimataifa ,msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Misri ameelezea masikitiko yake juu ya kumalizika muda wa makubaliano hayo ya amani akisema kwamba wapalestina ndio watakaoumia zaidi.

Rais Mahmoud Abbas anatazamiwa kujadiliana na rais Bush juu ya hali ilivyo katika gaza mjini Washington hii leo.Abbas ametoa mwito wa kurefushwa kwa muda huo wa makubaliano ya amani lakini hana mamlaka ya eneo hilo la ukanda wa Gaza tangu pale Hamas ilipovitimua vikosi vyake na kuchukua udhibiti wa eneo hilo mwezi juni mwaka 2007.Kwa upande mwingine Israeli imeshasema kwamba itachukua hatua kuambatana na hali itakavyokuwa.Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika jeshi la Israel amesema watadumisha utulivu ikiwa pia upande wa Gaza utafanya hivyo na kuongeza kusema kwamba vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vinauwezo wa kuharibu miundo mbinu yote katika Gaza lakini hatua hiyo itachukuliwa tu ikiwa hawana budi na kutakapokosekana uungwaji mkono wa kimataifa.

Tayari makundi ya wanamgambo wakipalsetina wanaoendesha shughuli zao katika ukanda wa gaza wameshaanza kuongeza nguvu mashambulio yao ya roketi dhidi ya eneo la kusini mwa Israeli katika muda wa siku kadhaa zilizopita.

Mapema hii leo wanamgambo hao walivurumisha roketi mbili katika mji wa Eshkol kusini mwa Israeli.Hali ya wasiwasi imeongezeka ndani na nje ya Gaza hii leo baada ya kundi la Hamas kutangaza msimamo wao wa kutokubali kurefusha muda wa makubaliano ya kusitisha vita ambayo tangu hapo yamekuwa yakiregarega.Pande zote mbili Hamas na Israeli zimeonya kwamba ziko tayari kujibu mashambulio ikiwa zitashambuliwa.

Vyombo vya habari ndani ya Israeli vinaendelea kutangaza kujiweka tayari kwa vikosi vya usalama pamoja na waisreli wanaoishi katika maeneo yaliyo karibu na ukanda wa gaza.Kwa upande mwingine waziri wa ulinzi wa Israeli Ehud Barack amesisitiza kwamba haoni haja ya kunazisha opresheni kubwa ya kijeshi katika Gaza.

Makubaliano ya kusitisha vita yamekuwa katika hali ngumu tangu yalipofikiwa mwezi juni tarehe 19 huku ghasia zikiongezeka tangu mwezi Novemba ambapo wapalestina 18 waliuwawa wakati Israeli ikishambuliwa na zaidi ya maroketi 250 na makombora kutoka Gaza.

Aidha mashirika ya kutoa misaada ya Umoja wa mataifa yanasema kwamba yameshindwa kusambaza msaada wa chakula kwa kiasi cha watu millioni moja na nusu katika Gaza kufuatia kufungwa kwa mipaka pamoja na mashambulio ya maroketi.