1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makao makuu ya polisi yashambuliwa Pakistan

27 Mei 2009

Shambulio la bomu lililofanywa dhidi ya makao makuu ya polisi katika mji wa Lahore nchini Pakistan,limeua watu wasiopungau 30 na kujeruhi zaidi ya 200 wengine.

https://p.dw.com/p/HyFg
Pakistani security officials and rescue workers gather at the site of suicide car bombing in Lahore, Pakistan on Wednesday, May 27, 2009. Gunmen detonated a car bomb near police and intelligence agency offices in Lahore on Wednesday, killing about 30 people and wounding more than 100 in one of Pakistan's deadliest attacks this year, officials said. At least four men with rifles stepped from the car and opened fire on the intelligence agency building, then set off a massive blast when security guards returned fire, officials said. (AP Photo/K.M. Chaudary)
Polisi na wasaidizi wakisaka eneo lililoteketezwa katika shambulio la bomu mjini Lahore.Picha: AP

Hakuna aliedai kuhusika na shambulio la Lahore lililofanywa wakati Mkuu wa Majeshi ya Marekani,Jemadari David Petraeus akiwa mji mkuu wa Pakistan Islamabad kukutana na viongozi wa serikali na jeshi. Pakistan inahimizwa na Marekani kuchukua hatua kali za kijeshi dhidi ya wanamgambo kaskazini-magharibi ya nchi hiyo kuwangoa wafuasi wa al-Qaeda na kukomesha msaada unaotolewa kwa wanamgambo wa Taliban katika nchi ya jirani Afghanistan.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Rehman Malik alipozungumza na waandishi wa habari leo hii alisema, anaamini kuwa wapinzani wa Pakistan wanaotaka kuleta vurugu nchini humo na kuzia ushindi wa majeshi katika Bonde la Swat, sasa wanalenga miji.Shambulio la leo mjini Lahore limesababisha hasara kubwa ya majengo huku hospitali zikiripoti kuwa kama watu 30 wameuawa na zaidi ya 200 wamejeruhiwa. Watu walioshuhudia shambulio hilo wanasema, muda mfupi kabla ya bomu kuripuka watu wanne wenye silaha walitoka kwenye gari na wakaanza kuwafyetulia risasi walinzi kwenye lango la makao makuu ya polisi.

Lahore ni mji mkuu wa Wilaya ya Punjab iliyo tajiri sana na ina wakaazi wengi kabisa nchini humo. Mji huo mkubwa wa pili vile vile, ni makaazi ya maafisa na viongozi wa kijeshi wa ngazi za juu. Katika miaka ya hivi karibuni, mji wa Lahore umeshuhudia idadi kadhaa ya mashambulio ya bomu lakini wakaazi wake walihisi kuwa huko kuna usalama zaidi kuliko katika miji mingine ya Pakistan. Lakini hali hiyo ilibadilika baada ya wanamgambo hapo Machi 30, kuthubutu kushambulia shule inayotoa mafunzo kwa polisi. Shambulio hilo liliua makuruti wanane na wengi wengine walijeruhiwa. Kiongozi wa Taliban nchini Pakistan, Baitullah Mehsud alidai kuhusika na shambulio hilo ambalo lilitokea majuma machache tu baada ya wanamgambo wenye silaha kushambulia basi lililokuwa likiwasafirisha wachezaji wa timu ya kriket ya Sri Lanka mjini Lahore. Dreva wa basi na polisi sita waliuawa katika shambulio hilo.

Tangu katikati ya mwaka 2007, mashambulio ya wanamgambo yameongezeka nchini Pakistan na hasa hulenga wanajeshi, majengo ya serikali na vituo vya nchi za magharibi. Maafisa wa Pakistan walikwisha onya juu ya uwezekano wa kutokea mashambulio ya wanamgambo kulipizia kisasi operesheni ya kijeshi inayoendelea katika Bonde la Swat. Katika operesheni hiyo, kiasi ya wanajeshi 15,000 wanapambana na wanamgambo wanaokadiriwa kuwa ni kati ya 4,000 na 5,000.

Mwandishi: P.Martin - (RTRE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman