1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamo waziri mkuu wa utawala wa Sadam Hussein,Tareq Aziz ahukumiwa adhabu ya kifo

Oumilkher Hamidou26 Oktoba 2010

Mahakama kuu ya Iraq yawakuta na hatia vigogo watatu wa utawala wa zamani wa Irak kwa makosa miongoni mwa mengineyo ya uhalifu dhidi ya ubinaadam-mahakama hiyo yaamuru wanyongwe

https://p.dw.com/p/PoTn
Tarek Aziz akisikiliza kesi dhidi yake mnamo mwaka 2009Picha: AP

Mahakama kuu ya Iraq imemhukumu adhabu ya kifo makamo waziri mkuu wa zamani wa Iraq,Tarek Aziz, kwa kuchangia kukandamizwa jamii ya washiya katika miaka ya 80.

"Korti kuu ya Iraq imetoa amri ya kunyongwa Tarek Aziz kwa mchango wake katika kufyekwa vyama vya kidini" -hayo lakini ni kwa mujibu wa televisheni ya taifa Al Irakiya.

Vigogo wawili wengine wa utawala wa zamani wa Saddam Hussein,waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Saadoun Shaker, na katibu wa zamani wa Sadam Hussein, Abid Hamoud, nao pia wamehukumiwa adhabu ya kifo hii leo.

Wamekutikana na hatia ya kushiriki katika opereshini ya kuwakandamiza washiya baada ya njama ya kutaka kumuuwa Sadam Hussein mwaka 1982 katika mji wa Doujail, kaskazini mwa mji mkuu Baghdad.

"Uamuzi huu umesababishwa na madhila dhidi ya vyama na wakuu wa madhehebu ya shiya katika miaka ya 80 wakati wa vita dhidi ya Iran- akiwemo Mohammed Baqr Sadr, aliyeuliwa pamoja na dada yake April tano mwaka 1980" , amesema hayo msemaji wa korti kuu, Mohammed Abdoul-Saheb, alipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Baqr Sadr ni muasisi wa chama cha Da' wa cha waziri mkuu anaemaliza wadhifa wake, Nouri al Maliki.

"Hukmu hii imelengwa kulipiza kisasi dhidi ya yeyote aliyekua na mafungamano na enzi za zamani nchini Iraq", amesema kwa upande wake mtoto wa kiume wa mhukumiwa, Ziad Aziz, akiwa mjini Amman, Jordan, ambako familia ya Aziz imekua ikiishi tangu Marekani ilipoivamia Irak mnamo mwaka 2003.

"Kesi hii si chochote chengine isipokua kiroja tuu" -amesema wakili wa Tarek Aziz, Giovanni de Stefano.

Wahukumiwa wana muda wa siku 30 kukata rufaa.

Kwa mujibu wa sheria za Irak, hukmu ya kifo inabidi kwanza iidhinishwe na tume ya rais kabla ya kutekelezwa.

Tarek Aziz, mwenye umri wa miaka 74, ambae July mwaka huu alihamishwa kutoka kambi ya kimarekani ya Cropper na kupelekwa katika jela ya Kazimiya, tokea hapo anatumikia kifungo jumla cha miaka 22 kwa makosa ya kuhusika na mauwaji ya dazeni kadhaa za wafanya biashara mnamo mwaka 1992 pamoja pia na kuhamishwa kwa nguvu Wakurd kaskazini mwa nchi hiyo.

Tangu September iliyopita wakili wa Tarek Aziz amekua akisema serikali ya Iraq inafikiria uwezekano wa kumuachia huru kutokana na sababu za afya. Lakini mtu wakaribu wa waziri mkuu wa Irak amekanusha ripoti hizo.

Hukmu ya kifo dhidi ya Tarek Aziz imelaaniwa vikali na halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya.

Msemaji wa muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema tunanukuu: "Msimamo wetu kuhusu adhabu ya kifo unajulikana. Mwisho wa kumnukuu.

Habari za kuaminika kutoka Brussels zinasema bibi Ashton anapanga kuwaelezea viongozi wa Irak msimamo wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir/afp,reuters

Mpitiaji: Miraji Othman