1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majaribioya maroketi ya Iran

Miraji Othman11 Julai 2008

Wasiwasi duniani kuhusu majaribio ya maroketi ya Iran

https://p.dw.com/p/EaOt
Rais wa Iran, Mahmoud AhmadinejadPicha: ISNA

Jamii ya kimataifa imeyaangalia kwa wasiwasi majaribio ya karibuni ya maroketi ya masafa ya kati na marefu yaliofanywa na Iran. Hasa Israel imesema itachukua hatua pindi usalama wake utakuwa hatarini. Lakini vipi mtu kweli anaweza kukitathmini kitendo hicho cha viongozi wa Iran cha kutunisha misuli yao? Jee kitendo hicho ni cha kuonesha ubabe au ni uchokozi wa makusudi?


Kiini cha sakata hii ya majira haya ya kiangazi kinabakia juu ya lile suali, kama eneo hilo litasukumwa na Iran kwenye mzozo wa kijeshi au Iran inajionesha tu ubabe ili kuwashughulisha tena wanasiasa na pia vyombo vya habari. Hata kidogo hakuna tathmini ya aina moja, mtu akiangalia matamko yaliotolewa siku chache zilizopita baada ya Iran kufanya majarabio ya maoroketi yake. Matamshi ya wanasiasa na mabingwa wa nchi za Magharibi na Israel yanazungumzia juu ya uchokozi mpya wa Iran na hata kughushiwa na kuongozwa kwa kompyuta zile picha zilizoonyesha kufyetuliwa maroketi hayo. Lakini watu wote walikubaliana juu ya jambo moja, nalo ni kuionya Iran isiendelee kuchezea moto na kuifanya hali ya mambo izidi kuwa mbaya.


Lakini maombi hayo yangekuwa yana haki pale katika siku zilizopita takwa kama hilo lingetumwa kuelekea anwani nyingine; kwa mfano, pale makamo wa waziri mkuu wa Israel, Shaul Mofaz, alipotishia wazi wazi kwamba Israel itaishambulia Iran. Au pale muda mfupi baadae Israel ilipojinata wazi wazi na kufanya luteka kubwa ya jeshi lake la anga kusini mwa Ugiriki kuonesha vipi inavoweza kuishambulia Iran kutoka angani. Pia Wamarekani na Waengereza walichochea pale walipofanya luteka ya jeshi la majini katika Ghuba la Uajemi, huku mbinyo zaidi ukiwekwa huko Marekani kutaka bunge la nchi hiyo likubali Iran izingirwe, hatua ambyo itakaribia kama kutangaza vita dhidi ya nchi hiyo.


Kutokana na hatua zote hizo hakujasikika malalamiko wala hakujaeklezewa wasiwasi. Bila ya shaka hakujakuweko na ushahidi kwamba Iran kwa miaka imekuwa ina maroketi haya yaliofyetuliwa hivi karibuni. Lakini kinachojulikana, na jambo ambalo halijawahi kulalamikiwa, ni kwamba Israel imekuwa na maroketi kama hayo kwa miaka 20 sasa na na imetengeneza chapa ilio bora zaidi na yenye kufikia masafa ya kilomita alfu sita hadi saba. Haya yote, lakini, yanamalizikia katika jambo moja, nalo ni kumtafuta nani aliye mkorofi. Hakuna ushahidi, lakini inapokuja Iran dhana na shuku zinatosha ili kuifanya nchi hiyo ipige magoti. Na inasikitisha kwamba kinachofuata ni sarakasi ya kuonya kushambuliwa Iran au nchi hiyo kujionesha kwamba iko tayari kujilinda. Hali hiyo ya kutoelewana haitokani na haiendelei kwa sababu ya nia ovu, lakini inachochewa na yale mashambulio mepya ya maneno yanayotolewa na Rais wa Iran dhidi ya Israel na Marekani. Kutokana na kitendo hicho, Mahmoud Ahmadinejad vivyo hivyo, tena kila mara, amekuwa akiluamiwa ndani ya Iran kwenyewe. Kwa hivyo watu huko Marekani na Israel na pia hapa Ujerumani lazima watambuwe kwamba wanawavunja moyo hao watu wanaomlaumu Mahmud Ahmadnejad na kuwapa nguvu wenye vichwa ngumu huko Iran ikiwa itafuatwa hiyo njia inayoangalia upande mmoja tu kuelekea Iran.