Majadiliano katika bunge la Libanon juu ya kupata rais mpya wa nchi hiyo | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Majadiliano katika bunge la Libanon juu ya kupata rais mpya wa nchi hiyo

Bunge la Lebanon, kwa hakika, lililazimika leo lichaguwe rais mpya wa nchi hiyo. Lakini upande wa serekali na ule wa upinzani zinabishana, kwa hivyo hakutegemewi kwamba kutakuweko masikilizano.

Rais wa Libanon, Emile Lahoud(kushoto), na Rais wa Syria, Bashar al-Asad

Rais wa Libanon, Emile Lahoud(kushoto), na Rais wa Syria, Bashar al-Asad

Pale kipindi kilichowekwa na sheria kwa Rais wa Libanon, Emile Lahoud, kilipomalizika katika majira ya mapukitiko ya mwaka 2004, Syria ilitumia misuli yake na ikalilazimisha bunge la Libanon lifanye mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo. Iliamuliwa kwamba kipindi cha rais huyo kirefushwe kwa miaka mitatu. Miaka hiyo mitatu sasa inakwisha, na hali ya mambo, kimsingi, imebadilika kabisa. Kwanza kabisa ni kwamba majeshi ya Syria hayako tena Libanon, na kwa hivyo haiwezi tena kuiona nchi hiyo kama sehemu ya ardhi yake. Hadi leo Syria bado inaifikiria Libanon kuwa ni sehemu ya ardhi yake.

Na katika miaka mitatu iliopita kuna mambo yaliobadilka huko Libanon. Baada ya kuuliwa mwanzoni mwa mwaka 2005 yule waziri mkuu aliyekuwa analeta mabishano, Rafik al-Hariri, muungano wa Wakristo, Wasunni na wa-Druze wanaopendelea siasa za Magharibi, ukiwa pamoja na waziri mkuu, Fuad Siniora, unajaribu kuikwamua Libanon kutoka kwenye mtego wa matatizo ya Mashariki ya Kati, hali ambayo imekuwa ikiiumiza nchi hiyo kwa muda mrefu.. Kujiingiza Israel kusini mwa nchi hiyo, hadi kuendesha vita vilivo wazi, kama ilivotokea mwaka jana, kujiingiza Syria na Iran upande wa mashariki pamoja na mizozo ya ndani ya nchi hiyo ambayo inasamabaa hadi katika kambi ya Wakristo, kambi ambayo sasa haijaungana tena kama ilivokuwa zamani.

Muungano ulioko nyuma ya waziri mkuu Siniora una wingi mdogo sasa katika bunge la watu 128 katika nchi hiyo. Chama cha Hizbollah cha Washia pamoja na wafuasi wa Jenerali mstaafu, Michel Aoun, kwa karibu mwaka sasa kinajaribu kuiangusha serekali inayoiona inaelemea kambi ya magharibi inayoipinga Syria. Lakini hadi sasa hawajafanikiwa. Lakini sababu nyingine ambayo inaudidimiza chini msimamo wa serekali ya waziri mkuu Siniora ni kwamba wingi wake bungeni umepungua kwani kila wakati wanauliwa wanasiasa walio katika kambi hiyo. Mara ya mwisho ilitokea siku chache zilizopita.

Serekali ya Lebanon inaiona Syria kuwa ndio dhamana ya mauaji hayo, japokuwa Syria nayo kwa hasira inakanusha jambo hilo. Na sasa pia rais Emile Lahoud, mtu anayeungwa mkono na Syria, amekuwa na wasiwasi. Kila wakati pale mtu anapotaka yafanyike maendeleo huko Beirut, kunatokea mauaji kama hayo na mwenendo wa kuirejesha hali kuwa ya kawaida unachafuliwa.

Emile Lahoud haibebeshi Syria dhamana ya hayo yanayotokea, lakini anajuwa thama kwamba hali ya mambo polepole inaweza kusambaa, jambo ambalo litakuwa kwa maslahi ya Syria. Hadi Novemba 24 muhula wa Emile Lahoud kubakia madarakani unamalizika, na lazima kupatikane muwafaka juu ya nani atachukuwa mahala pake. Mwanzoni ilipangwa kufanywe leo uchaguzi wa rais ndani ya bunge, lakini sasa haitakuwa hivyo. Upande wa serekali pamoja na upinzani zimekuwa zikibishana, na sasa ni wazi kwamba hakutapatikana wingi wa thuluthi mbili bungeni kuweza kumchagua rais mpya. Badala yake sasa kunatafutwa mtetezi wa suluhu kwa ajili ya wadhifa huo, na jambo hilo ndilo litatawala katika kikao cha leo. Lakini rais mpya huenda akachaguliwa baada ya kupita wiki fulani kutoka sasa.

 • Tarehe 24.09.2007
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7q
 • Tarehe 24.09.2007
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7q

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com