1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahmoud Abbas azuru makao makuu ya Umoja wa Ulaya

Zainab Aziz
22 Januari 2018

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanajiandaa kuanza majadiliano juu ya jitihada za kuanzisha upya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Mahmoud Abbas autaka Umoja wa Ulaya ulitambue dola la Palestina.

https://p.dw.com/p/2rHNw
UK Brexit - House of Commons - EU Flagge
Picha: picture alliance/NurPhoto/A. Pezzali

Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kutoa maombi hayo wakati atakapokutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya hii leo Jumatatu mjini Brussels, Ubelgiji.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya bibi Federica Mogherini alipowasili kwenye eneo utakapofanyika mkutano huo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba suala la Jerusalem ni mapungufu katika Nyanja za kidiplomasia na kuongeza kwamba mji huo unapaswa uwe mji mkuu wa mataifa mawili.

Federica Mogherini Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya
Federica Mogherini Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Bibi Mogherini amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono mfumo wa kimataifa katika kufanikisha mazungumzo ya moja kwa moja baina ya pande mbili za Israel na Palestina. Amesema wamekuwa wakijadiliana na Marekani kupitia kundi la pande nne katika kutatua mzozo wa mashariki ya Kati.

Waziri wa mambo ya nje wa Palestina Riad al-Malk amesema kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ataueleza Umoja wa Ulaya uchukue hatua za kukabiliana na uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Hata hivyo baadhi ya wanadiplomasia mjini Brussels wamesema kuitambua Palestina kama taifa sio suala litakalozungumziwa leo hii. Ziara ya Mahmoud Abbas inafanyika wakati ambapo makamu wa rais wa Marekani Mike Pence anazuru Israel katika ziara yake ya eneo la Mashariki ya kati.

Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas
Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: Getty Images/AFP/F. Mori

Wiki iliyopita, Abbas alizipinga jitihada za Trump katika kutatua mgogoro wa muda mrefu wa Mashariki ya Kati akisema hilo ni pigo la karne na ambalo limesababisha mfadhaiko kwa kusema kwamba Israel imeuzamisha mkataba wa Oslo ambao unaimarisha mchakato wa amani uliokwama.

Mahmoud Abbas na utawala wa Palestina umekataa kukutana na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence kutokana na tamko hilo la Marekani na kuifanya ziara yake iwe tofauti kutokana na kuwa kiongozi wa ngazi ya juu wa Marekani anazuru eneo hilo bila kukutana na Wapalestina.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/DPAE

Mhariri:Iddi Ssessanga