1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahmoud Abbas aondowa uwezekano wa kuzungumza na Hamas

Oummilkheir21 Juni 2007

Pirika pirika za kuufufua utaratibu wa amani ya mashariki ya kati katika wakati ambapo ufa unazidi kua mpana kati ya Fatah na Hamas

https://p.dw.com/p/CB3R
Waziri mkuu wa Israel na rais George W. Bush
Waziri mkuu wa Israel na rais George W. BushPicha: AP

Rais wa Utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas ameondowa uwezekano wa kuzungumza na Hamas anaowatuhumu walitaka kumuuwa na kufanya mapinduzi huko Gaza.

“Sitozungumza na makatili,watu waliofanya mapinduzi” amesema hayo rais Mahmoud Abbas mbele ya wakuu wa chama chake cha Fatah katika ukingo wa Magharibi.Amemshutumu pia mkuu wa tawi la kisiasa la Hamas anaeishi uhamishoni mjini Damascus, Khaled Mechaal kuhusika na njama ya kutaka kumuuwa.



Mahmoud Abas aliyeivunja serikali ya umoja wa taifa iliyoundwa na Fatah na Hamas,na kuamuru iundwe serikali ya dharura ambayo madaraka yake yanatuwama ukingo wa magharibi tuu,ametoa mwito hata hivyo wa mshikamano huko Gaza.

“ Nawatolea mwito ndugu zetu wa Gaza,nawaambia mbinu za makatili hao wafanya mapinduzi hazina hatima njema-tutaendelea kushirikiana “ ameshadidia kiongozi huyo wa utawala wa ndani.

Maelfu ya wapalastina waliteremka majiani baada ya hotuba hiyo na kutia moto picha zinazofanana na kiongozi huyo wa utawala wa ndani wanaemtuhumu kua “kibaraka wa Marekani.”

Kutokana na mtihani uliopo,kuna wanaoashiria uwezekano wa kila upande, Gaza na Ukingo wa magharibi kufuata njia yake na kufika hadi ya kuibuka mataifa mawili madogo ,jambo ambalo linaweza kuirahishia mambo Israel katika juhudi zake za kutaka yafufuliwe kwa masharti mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati.

Israel inajaribu kuhakikisha Hamas wanatengwa kisiasa,kiuchumi na kijeshi katika Ukanda wa Gaza.Dola hilo la kiyahudi na washirika wao mjini Washington wameelezea utayarifu wao wa kuiunga mkono serikali ya dharura iliyotangazwa na rais M ahmoud Abbas katika Ukingo wa Magharibi baada ya serikali ya umoja iliyokua ikidhibitiwa na Hamas kuvunjika.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmud Abbas huenda wakakutana hivi karibuni nchini Misri kuzungumzia hali namna ilivyo katika maeneo ya utawala wa ndani na uwezekano wa kuufufua utaratibu wa amani.

Rais George W. Bush wa Marekani anasema:

„Nataraji viongozi wa eneo hilo wanaelewa kuna njia ya kufikia amani.Rais Mahmoud Abbas wa Palastina kwa mfano na tungependelea kuona ulimwengu wa kiarabu pia ukiunga mkono mpango huo.

Pande nne zinazosimamia utaratibu huo wa amani ya mashariki ya kati,ambazo ni Marekani,Urusi,Umoja wa mataifa na Umoja wa ulaya,wanapanga kumteuwa mjumbe maalum ambae jukumu lake litakua kusimamia mazungumzo kati ya Israe na wapalastina na kuunga mkono juhudi za amani za mataifa ya kiarabu.Miezi ya hivi karibuni,maafisa wa serikali ya Marekani wamekua wakizungumzia uwezekano wa kukabidhiwa wadhifa huo Tony Blair atakaeng’atuka wiki ijayo kama waziri mkuu wa Uengereza.

Wakati huo huo mamia ya wapalastina waliokua wamekwama katika kivukio cha Erez kati ya Israel na Gaza wamehamishiwa Misri.Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita mamia ya wapalastina wanachama wa Fatah na vikosi vya usalama walikimbilia Erez wakihofia kisasi cha wafuasi wa Hamas wanaolidhibiti eneo la Gaza tangu June 15 iliyopita.