1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, kutoa uamuzi wake leo kuhusu Rais wa Sudan.

Halima Nyanza/AFP4 Machi 2009

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, leo inatoa uamuzi wake kuhusiana na kushtakiwa kwa Rais wa Sudan Omar Al Bashir kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/H5GV
Rais wa Sudan Omar Al Bashir, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita leo inatarajia kutoa uamuzi wa kutoa kibali cha kukamatwa kwake, kwa shutuma za uhalifu wa kivita.Picha: AP Photo

Uamuzi huo umepangwa kutolewa leo na majaji wa mahakama hiyo wakati wa mkutano na Waandishi wa habari mjini The Hague, Uholanzi, ambako Rais Omar Al Bashir anakabiliwa na uwezekano wa kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi, kushtakiwa katika mahakama hiyo tangu ilipoanza kufanya kazi mwaka 2002.


Rais A Bashir mwenye umri wa miaka 65, ambaye waendesha mashtaka wanasema aliwaagiza wanajeshi na wanamgambo nchini humo kuteketeza jamii ya makabila matatu yanayoshiriki katika uasi katika jimbo hilo la Darfur, amepuuzia tuhuma hizo dhidi yake.


Akizungumza jana mjini Khartoum, Rais huyo wa Sudan amesema uamuzi wowote utakaotolewa na Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita hauna manufaa kwao.


Kwa upande wake Mwendesha Mashtaka Mkuu katika mahakama hiyo Luis Moreno Ocampo, ambaye Julai mwaka uliopita, alitoa pendekezo la kutolewa kibali cha kukamatwa Rais Bashir, amesema ana ushahidi wa kutosha dhidi ya kiongozi huyo wa nchi kubwa barani Afrika.


Ameongezea kusema kuwa wana mashahidi tofauti zaidi ya 30, ambao wataelezea jinsi kiongozi huyo alivyodhibiti kila kitu.


Luis Moreno Ocampo anamshutumu Rais Bashir kwa kuyapa maelekezo majeshi yake kuangamiza makabila ya Fur, Masalit na Zaghawa na kusema kuwa watu milioni 2.5 waliathirika kutokana na hatua yake hiyo.


Mwendesha mashtaka mkuu anamshutumu kiongozi huyo wa Sudan kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na mauaji ya halaiki.

Chini ya waraka wa Roma, Mwendesha mashtaka hamshtaki mtu, natoa pendekezo kwa majaji kwa majaji , Wanaweza kukubaliana na ombi langu na wanaweza kulitupilia mbali au wanaweza kutaka ushahidi zaidi, kwa hiyo majaji ndio wenye mamlaka zaidi ya kuamua....''


Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita haina mamlaka ya kulazimisha utekelezaji wa waranti wake yenyewe, lakini hutarajia kwamba mtuhumiwa anaweza kukamatwa akiwa katika ardhi ya mataifa ambayo yamesaini waraka wa Roma wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo.


Umoja wa Mataifa umesema watu laki tatu wameuawa tangu kuzuka kwa ghasia hizo katika jimbo hilo la Darfur lilioko magharibi mwa Sudan, mwaka 2003, wakati waasi kutoka katika makabila madogo walipochukua silaha katika kile walichodai juhudi za kudai haki, kugawana rasilimali na madaraka na utawala uliopo.


Mawaziri kutoka nchi za Kiafrika na Kiarabu, wameitaka mahakama hiyo ya Kimataifa kuchelewesha kutoa maamuzi yoyote ya kisheria dhidi ya Rais Bashir kwa ajili ya amani ya Darfur.


Katika hatua nyingine, kundi la waasi wa Darfur la Justice and Equality Movement -JEM-, limetishia kufikiria tena juhudi zake za kutaka kumpindua Rais Bashir, iwapo kibali cha kumkamata kitatolewa na kushindwa kuonesha ushirikiano.