1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magenge yashika doria katika mkoa wa bonde la ufa nchini Kenya

Josephat Charo3 Februari 2008

Upinzani wautaka Umoja wa Afrika upeleke walinda amani kukomesha mauaji

https://p.dw.com/p/D1k0
Raia wakiyakimbia machafuko ya kikabila magharibi mwa KenyaPicha: AP

Magenge ya wapiganaji waliokuwa wamejihami na marungu, magongo yaliyochongwa na mapanga yameshika doria hii leo katika barabara za mkoa wa bonde la ufa nchini Kenya.

Mamia ya watu wameyakimbia mashambulio ya kikabila kwenye misafara iliyokuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Polisi wamefyatua risasi angani kulitawanya genge moja lililokuwa likikilinda kizuizi cha barabarani ili kuruhusu basi lililokuwa limewabeba wakimbizi lipite.

Baadhi ya vijana waliokuwa na mishale ya sumu katika kizuizi hicho wamesema walikuwa wakilinda amani wakiwalaumu polisi kwa kuegemea upande mmoja na kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wananchi.

Matukio haya yametokea siku moja kabla mazungumzo ya kutafuta suluhisho kwa mgogoro wa kisiasa yanayoongozwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, yakitarajiwa kuingia awamu muhimu hapo kesho.

Hii leo upinzani nchini Kenya umeutaka Umoja wa Afrika upeleke wanajeshi wa kulinda amani kumaliza machafuko yanayoendelea nchini humo.

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, amesema chama chake kimejitolea kwa dhati kushiriki katika mazunguzo ya kutafuta suluhisho la kisiasa na kutaka mateso dhidi ya raia yakome.

Aidha kiongozi huyo amesema chama chake cha Orange Democratic movement, ODM, hakitajondoa katika mazungumzo hayo.