1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini

Quast, Ulrike 11 Februari 2008

Mvutano ndani ya jumuia ya kujihami ya magharibi NATO

https://p.dw.com/p/D5a1
Wanajeshi wa NATO nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/ dpa

Eti kweli jumuia ya kujihami ya magharibi NATO inazozana juu ya namna ya kugawana madaraka?Hilo ndilo suala kuu lililowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.


Marekani inashikilia majukumu yagawanywe sawa miongoni mwa wanachama wa NATO waliotuma wanajeshi nchini Afghanistan.Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates ameshadidia hayo katika mkutano wa usalama mjini Munich.Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linajiuliza kwa namna gani mzozo huu unaozidi kukua unaweza kuiathiri jumuia ya kujihami ya magharibi NATO na mchango wa Ujerumani nchini Afghanistan.


Hata kama, waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates amedai mjini Munich,eti hoja zake kutaka wanachama wote wa NATO wawajibike sawa nchini Afghanistan hazijalengwa pekee Ujerumani,hisia zimesalia pale pale,kila mmoja anaamini hoja hizo zinaihusu zaidi Ujerumani.Rais mpya wa Marekani hatoacha kuishinikiza serikali mjini Berlin ipeleke wanajeshi zaidi kwaajili ya mapigano kusini mwa Afghanistan.Madai hayo yasiwe sababu kwa Ujerumani kutozingatia kwa makini masilahi yake.Miongoni mwa hayo ni pamoja na kuepusha pasitokee mgawanyiko wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO  na kuepusha  zisishindwe shughuli za jumuia hiyo nchini Afghanistan.Mapambano dhidi ya magaidi wanaofuata itikadi kali ya dini ya kiislam yakishindwa nchini Afghanistan hali hiyo itahatarisha pia kwa njia moja au nyengine usalama wa Ujerumani.


Gazeti la HANDELSBLATT la mjini Düsseldorf linaandika:


Kumezuka ufa katika jumuia ya kujihami ya magharibi NATO.Upana wa ufa huo umebainika katika mkutano wa usalama mjini Munich.Wanasiasa wa Marekani wamekuja mkutanoni wakiwa na fikra ni mkutano wa kukusanya wanajeshi.Wanasiasa wa Ujerumani kwa upande wao wanajishughulisha zaidi na namna ya kuimarisha sera za usalama.Si hasha kwa hivyo kama pande hizi mbili hazielewani."


Hata STUTTGARTER ZEITUNG linahisi kuna hatari inayoikabili jumuia  ya kujihami ya magharibi NATO.


NATO inajikuta njia panda.Na Ujerumani ndio hivyo hivyo.Mvutano wa kugawana majukumu nchini Afghanistan unabainisha hali namna ilivyo.Watu wamejipatia muda kidogo kufuatia mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya NATO mjini Vilnius, na pia kufuatia mkutano wa usalama mjini Munich- ingawa mijadala ilikua moto moto lakini mfarakano umeweza kuepukwa.Kilichosalia ni kusubiri mkutano wa kilele wa NATO utakaoitishwa wiki chache kutoka sasa mjinmi Bucharest ,ili kuweza kutambua kama jumuia hiyo ya kujihami ya magharibi inaweza kweli kuvumilia mivutano kwa muda mrefu na hatimae kuipatia ufumbuzi au la.Jukumu hilo naslo pia si dogo."