1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

1 Februari 2010

Mada kuu iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu ni suali iwapo ni sahihi kwa serikali kununua data za wakwepa kodi zilizoibiwa.

https://p.dw.com/p/Lobv
Mada nyingine ni pendekezo la kuanzisha kitivo cha theolojia ya Kiislamu katika vyuo vikuu nchini Ujerumani.Basi tutaanza na gazeti la BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN linalosema: "Wakwepa kodi ni wahalifu - kwa hivyo serikali, kwa niaba ya wale walio waaminifu, inawajibika kufanya kila kiwezekanacho kuwapata wahalifu hao. Isipofanya hivyo, basi itakuwa sawa na kuwaruhusu wakwepa kodi kuficha fedha hizo haramu kwenye akaunti za siri nje ya nchi. Waziri wa Fedha hana budi ila kuzilipia data za wahalifu hao na baadae wizara yake itajipatia kitita cha pesa. Hatua hiyo iwe somo kwa wengine." Gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT likiendelea na mada hiyo hiyo linauliza: "Je, serikali ya Ujerumani ilipe Euro milioni mbili na nusu kujipatia data za akaunti katika benki ya Uswisi? Jawabu ni wazi "Ndio." Si kwa sababu tu kuwa serikali baadae itajipatia pesa za kodi. Kilicho muhimu zaidi ni kuhifadhi mfumo wa haki wa malipo ya kodi. Kwani mtindo wa kununua habari, si jambo geni tena panapokuwepo haja ya kuchunguza uhalifu. Kwa hivyo utaratibu huo kwa nini usitumiwe kuwakamata wanaoshukiwa kukwepa kodi?" Kwa maoni ya BILD ZEITUNG mfumo wa kodi nchini Ujerumani unatatanisha na kodi ni kubwa mno, lakini hizo si sababu za kufanya udanganyifu. Likiendelea linasema: "Asielipa kodi ni kupe, kwani anawaaachia wengine kulipia huduma za jamii. Mara nyingi wakwepa kodi ni matajiri wanaozungumza kwa ndimi mbili. Wanaficha fedha zao Uswisi na wakati huo huo wanapaza sauti kuwa wapokea misaada ya serikali ni wavivu wasiotaka kufanya kazi. Sasa serikali ina fursa ya kununua data zilizoibiwa za zaidi ya watu 1,500 waliotorosha pesa zao." MÜNCHNER MERKUR lakini linauliza iwapo ni sahihi kwa serikali kuwa mnunuzi wa mali ya wizi? Sasa tukitupia jicho mada nyingine gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG linasifu pendekezo la kutoa mafunzo kwa walimu wa dini ya Kiislamu huku Ujerumani. "Si busara tu kuwafunza walimu hao humu nchini bali ilipaswa kufanywa hivyo tangu muda mrefu. Hadi sasa, walimu wa dini ya Kiislamu walitoka nchi za nje na hasa Uturuki. Je, walimu hao wanafahamu kwa umbali gani maisha ya Waislamu nchini Ujerumani? Wakati umewadia kuwapa nafasi Waislamu wanaoishi Ujerumani kusomea dini yao kwa matumaini kuwa walimu hao watakuwa muhimu kuleta maelewano kati ya dini mbali mbali." Gazeti la SÜDKURIER pia linaunga mkono uamuzi wa Baraza la Sayansi na Elimu na kusema kuwa hiyo ni hatua sahihi kwa sababu mbali mbali: "Kwanza ni kwamba jamii ya Ujerumani ni mchanganyiko wa makabila na dini mbali mbali. Idadi ya Waislamu inaongezeka nchini - kwa hivyo ni dhahiri kuwa hali hiyo pia itambuliwe katika masomo yanayotolewa katika vyuo vikuu. Anaetaka kuwajumuisha Waislamu katika jamii ya Ujerumani,asiyachie masomo ya dini mikononi mwa walimu wanaotoka nje na ambao mara nyingi hawafahamu hata neno moja la Kijerumani." Mwandishi: Martin, Prema/DPA Mhariri: M.Abdul-Rahman