1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

28 Desemba 2009

Jaribio lililoshindwa la kutaka kuiripua ndege ya Marekani, mapambano mapya kati ya polisi na wapinzani wa serikali nchini Iran ni habari zilizotawala safu za mbele katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/LEt6

Tutaanza na gazeti la HESSISCHE ALLGEMEINE linalosema:

"Ukweli kuwa abiria aliweza kupita vituo vyote vya ukaguzi na kuingia ndani ya ndege akiwa na miripuko umedhihirisha udhaifu wa mfumo wa usalama na kwamba wanaosimamia ukagauzi hawawezi kutegemewa au teknolojia ya vyombo vya ukaguzi ina dosari. Bila shaka kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka, kuziba pengo lo lote lile la usalama lililokuwepo."

Likiendelea gazeti hilo linasema:

"Kinachotia wasiwasi ni kuwa Mnigeria Umar Faruk Abdulmutallab amekulia katika maisha ya neema,amesoma Uingereza lakini ameishia kuwa na itikadi kali za Kiislamu. Je, kuna wangapi wengine walio na misimamo kama hiyo linauliza gazeti la HESSISCHE ALLGEMEINE."

Kwa maoni ya SCHWÄBISHE ZEITUNG jaribio la Detroit linathibitisha kuwa pana haja ya kuwepo mawasiliano, kwani baba mzazi wa kijana huyo wa Kinigeria alikwisha watahadharisha maafisa kuhusu mwanae na kijana huyo alinyimwa ruhusa ya kuingia Uingereza.

Lakini ionekanavyo, habari hizo zote hazikuwafikia maafisa wa Kimarekani, licha ya kudhibiti teknolojia mpya kabisa ya upelelezi. Au labda orodha ya washukiwa ni ndefu mno? kwani zaidi ya watu nusu milioni wamo katika orodha ya Marekani. Basi suluhisho si kutupia jicho tu orodha ya majina bali kuyapitia majina hayo kwa makini zaidi.

Gazeti la SAARBRÜCKEN ZEITUNG kwa upande wake linakwenda umbali wa kushauri hivi:

"Mbali na kuwa na vyombo vya kisasa vya ukaguzi kwenye viwanja vya ndege na kuweka orodha ya washukiwa,wakuu wa usalama wanaweza kuchukua hatua zingine zisizogharimu pesa nyingi lakini zitakazosaidia. Miongoni mwa hatua hizo ni kuwazua abiria kuingia ndani ya ndege na mifuko ya mkononi, isipokuwa kwa dawa au vitu vinavyohitajiwa na watoto wakati wa safari. Tukio la Detroit litufunze moja: Usiwepo uzembe wa aina yo yote. Bado tunakabiliwa na kitisho cha ugaidi wa kimataifa."

Mada nyingine iliyochukua safu ya mbele magazetini ni mapambano yaliyozuka kati ya polisi na wapinzani wa serikali nchini Iran. Gazeti la SÜDWEST PRESSE limeandika:

"Serikali ya Iran inatumia nguvu kubwa kujaribu kuzima upinzani ulioibuka nchini humo. Ripoti chache zilizopatikana katika mtandao wa intaneti zinaonyesha ukatili wa viongozi waliomzunguka Rais Ahmedinejad. Risasi zimefyetuliwa na waandamanaji wamepigwa na vikosi vya usalama vinavyoiunga mkono serikali. Michafuko hiyo imeenea katika miji mingine pia na sio mji mkuu Tehran tu. Uchumi wa nchi umeporomoka na sasa Ahmedinejad alieahidi kunyanyua hali ya maisha ya umma sasa hawezi tena kutekeleza ahadi alizotoa. Sasa ndio serikali inajikuta katika hali ya kufa kupona."

Mwandishi:Martin,Prema /DPA

Mhariri: Othman,Miraji