1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

29 Julai 2009

Mkasa wa Waziri wa Afya wa Ujerumani Ulla Schmidt na gari lake la serikali lililoibiwa alikokwenda nalo mapumzikoni, ni mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/IzUH
FILE - The July 27, 2009 file photo shows Germany's health minister Ulla Schmidt, right greeting members of the public as she arrives on foot for a conference in Denia, Spain. Schmidt's official car that had been stolen last week has been found near Alicante on Wednesday, July 29, 2009. (AP Photo/Alberto Saiz)
Waziri wa Afya wa Ujerumani, Ulla Schmidt.Picha: AP

Kwa mfano, mhariri wa gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG kutoka Dresden anasema:

"Ulla Schmidt anafanya kosa lile lile, kama wanasiasa wengi waliomtangulia na waliojikuta katika hali kama hiyo. Yeye anashikilia kuwa hakuna kosa lililofanywa. Mwanasiasa huyo wa chama cha kisoshalisti SPD anashikilia kuwa hakuvunja sheria na wala haonyeshi kutia maanani sana hisia za umma. Angalionyesha unyenyekevu kidogo na kukubali kuwa amefanya kosa, basi mkasa huo ungesahauliwa baada ya siku chache. Kwa kuendelea kungángánia msimamo wake, waziri huyo anahatarisha pia mustakabali wake wa kisiasa."

Gazeti la WESTFÄLLISCHER ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linaandika hivi:

"Kwa kweli chama cha SPD juma hili, kilipanga kuanzisha kwa mbwembwe, kampeni yake ya uchaguzi. Lakini jitahada za wanasiasa waandalizi wa SPD Steinmeier na Münterfering hazikusaidia cho chote kwani mkasa wa Ulla Schmidt na gari lake la serikali lililoibiwa, umetia doa mpango huo na kwa sasa hakuna kinachoweza kufanywa kwa shamrashamra."

Mada nyingine kugonga vichwa vya habari magazetini leo hii, nchini Ujerumani ni tangazo la benki ya Ujerumani -Deutsche Bank- kuwa imepata faida kubwa katika sekta ya uwekezaji. Gazeti la KÖLNISCHE ZEITUNG linasema:

"Deutsche Bank inaweza kufurahia uamuzi wake wa kutojitenga na biashara ya uwekezaji,kwani hesabu zake mpya zinaonyesha kuwa kitengo cha uwekezaji kimeingiza faida ya takriban Euro bilioni 1 wakati biashara inayohusika na wateja binafsi ikipata faida ya Euro milioni 55 tu. Na kitengo cha mikopo, ndio kina wasiwasi kuwa kitendelea kuubeba mzigo wake kwa miezi kadhaa ijayo."

Homa ya mafua ya nguruwe inazidi kuzusha wasiwasi miongoni mwa umma nchini Ujerumani ambako tayari kama watu 4,000 wameambukizwa virusi vya homa hiyo. Sasa, mamilioni wanangojea chanjo ya kujikinga dhidi ya homa hiyo, utaratiibu huo ukitazamiwa kuanzishwa mwishoni mwa mwezi wa Septemba. Lakini tayari, kumezuka midahalo mikali juu ya suala, nani atakaesimamia gharama hizo. Gazeti la SÜDWEST PRESSE linauliza:

"Je, siku hizi nchini humu, hakuna kingine kinachozungumzwa isipokuwa suala la fedha? Kwani hata kabla ya chanjo hiyo kupatikana, mashirika ya bima za afya yameshaanza kuzungumzia gharama zake. Mtu atadhani kuwa maafisa hao ndio watakaotoa pesa hizo mifukoni mwao. Na wizara ya afya nayo wala haikukawia kueleza kuwa serikali, haiwezi kusimamia gharama za chanjo, kwani kwake, ni kweupe baada ya kutoa misaada mikubwa kwa benki na taasisi za fedha zilizoathirika kwa mtikisiko wa uchumi na fedha duniani. Kwa kweli, mdahalo kama huo unasikitisha."

Na kwa kumalizia, tunatupia jicho uhariri wa gazeti la CELLESCHE ZEITUNG kuhusika na sheria inayopiga marufuku kunywa pombe hadharani.Linaandika:

"Kwa hivi sasa mpango huo umegonga mwamba katika jimbo la Baden Württemberg, kwani kwa maoni ya wanasheria,kuwazuia watu kunywa pombe sehemu za hadharani ni hatua inayowanyima raia haki ya kuwa huru.Yaonekena kuwa jeribio la kuzuia ulevi hadharani kwa sasa limekwama. Je, huo ndio muhanga wa kuwa na uhuru lauliza gazeti la CEELISCHE ZEITUNG.

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman