1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

P.Martin4 Novemba 2008

Njama mpya ya baadhi ya wanachama wa Social Democrats-SPD-kumpinga kiongozi wa chama hicho mkoani Hesse,kuunda serikali ya mseto pamoja na chama cha mrengo wa shoto Die Linke ni mada iliyogonga vichwa vya habari hii leo.

https://p.dw.com/p/FnF4

Tunaanza na maoni ya gazeti la PASSAUER NEUE PRESSE linalosema:

"Yaonekana kana kwamba,Andrea Ypsilanti aliedhamiria kuunda serikali mpya katika mkoa wa Hesse na kumpiga kumbo Waziri Mkuu wa mkoa huo Roland Koch kwa njia yo yote ile,alishindwa kuona upinzani uliokuwepo katika chama chake mwenyewe.Chuki yake dhidi ya Koch kama sababu ya kungàngánia kuunda serikali ya mseto pamoja na chama cha Kijani na hata Die Linke kinachofuata sera kali za mrengo wa shoto,haikutosha kuleta umoja miongoni mwa wanachama wenzake mkoani Hesse na kuunda serikali hiyo kama alivyotazamia.Sasa kilichobaki ni kuitisha uchaguzi mpya katika mkoa huo.

Hata gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG linakubali kuwa njia pekee iliyokuwepo hivi sasa ni kuitisha uchaguzi mwingine mkoani Hesse. Likiendelea linasema:

Lakini ijulikane wazi kabisa kuwa chama cha SPD kitakujashindwa.Hata hivyo,ni bora kuitisha uchaguzi huo mapema iwezekanavyo ili chama hicho kisijekuaathirika hata katika uchaguzi mkuu hapo mwakani.Safari hii,Roland Koch huenda akaibuka mshindi mkoani Hesse lakini asijidanganye.Kwani yeye ndie alie sababisha hali hiyo ya mvutano.Ilimradi atabakia kiongozi wa chama cha CDU mkoani Hesse basi mtu anaweza kuwa na uhakika kwamba mazingira ya kisiasa katika mkoa huo hayatakuwa ya ustaarabu. Kwa vyo vyote vile,mkoa wa Hesse unastahili bora zaidi.

Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG likiendelea na mkasa wa SPD mkoani Hesse linasema:

Ni dhahiri kuwa mkasa huo una madhara makubwa hasa kwa chama cha SPD mkoani Hesse.Chama hicho kitahitaji muda mrefu mno kusafisha sifa yake.Lakini baya zaidi ni kwamba umma umepoteza imani yake katika siasa.Raia hawapendezwi na uchu wa wanasiasa kuwania madaraka.

Mada nyingine inayoendelea kugonga vichwa vya habari magazetini ni mgogoro wa fedha.Gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG linashangazwa kuona kuwa ni taasisi chache mno za fedha zilizojitokeza kupokea msaada kutoka serikalini,licha ya kuwepo mradi maalum wenye lengo la kuziokoa benki zilizoathirika katika masoko ya fedha duniani.

Lakini sasa Commerzbank,iliyo benki kuu ya pili nchini Ujerumani imejitokeza kuomba msaada wa serikali.Na kinyume ilivyodhaniwa,benki hiyo haikuadhibiwa bali kilichotokea ni kinyume kabisa.Kwani bei ya hisa zake zilipanda katika masoko ya hisa.Mara nyingine tena inadhihirika kuwa umma huukabili mgogoro wa fedha kwa mantiki kinyume na vile inavyozungumzwa miongoni mwa wataalamu wa kiuchumi,lamalizia NÜRNBERGER ZEITUNG.