1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

P.Martin3 Septemba 2008

Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatano ni machafuko ya kisiasa nchini Thailand na kampeni ya uchaguzi wa rais huko Marekani.

https://p.dw.com/p/FAYi

Tutaanza na gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG.Linasema,mapambano kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali nchini Thailand yadhihirisha mtengano mkubwa uliopo katika jamii.Likiendelea linasema:

"Masikini katika maeneo ya mashambani ambao kwa mara ya kwanza waliweza kuhakikishiwa maisha ya kimsingi na waziri mkuu wa zamani Thaksin aliepunduliwa,sasa wanajikuta wakipambana na umma unaotoka miji mikubwa.Wananchi hao wanaojiweza wanaandamana kuipinga serikali ya Waziri Mkuu Samak aliemrithi Thaksin.Tamko moja tu kutoka Mfalme Bhumibol anaeheshimiwa na wengi nchini humo lingesaidia kuzuia machafuko zaidi.Lakini Mfalme huyo anaeumwa amebakia kimya kabisa.

Kwa maoni ya gazeti la FINANCIAL TIMES la Ujerumani,uasi wa chama cha PAD nchini Thailand wala hauhusiki na demokrasia. Linaeleza: "Wanachokitaka waandamanaji hao si kuibadilisha serikali bali kubadilisha mfumo wa utawala.Yaani kiini cha madai yao ni mageuzi ya katiba-wanasema,theluthi moja ya wabunge ndio wachaguliwe na raia na wengine waliobaki wateuliwe.Jeribio la kubadili utaratibu uliopo,hulingana na mfumo unaofuatwa katika nchi za jirani Singapore,Malaysia au China.Wapinzani wa serikali ya Thailand wanadai kuwa uchumi wa nchi hizo umeweza kunyanyuka bila ya kupitia njia ya kidemokrasia.Lakini kuweka mbele maendeleo ya kiuchumi huenda kukaleta mafanikio ya muda mfupi tu-kwani hatimae nchini Thailand mivutano ya ndani itazidi kuongezeka."

Tukigeukia mada nyingine,BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linaeleza kuhusu kampeni za uchaguzi nchini Marekani.Linasema:

"Yaani Bristol,binti wa Sarah Palin mwenye miaka 17 ni mjaa mzito.Kwa hivyo miongoni mwa Waevanjelisti katika chama cha Republikan cha McCain,sifa ya Palin imeingia dosari.Lakini mpinzani wa kisiasa Barack Obama wa chama Demokrat,hakulipa umuhimu suala hilo:Kwa maoni yake, mambo yanayohusika na familia ni mwiko na hasa kuhusu watoto.

Lakini nchini Marekani,mambo yanakwenda kinyume na wakati wa sasa.Familia ya Palin sasa ni mzigo kwa McCain,kwani yeye hakujiarifu vya kutosha kuhusu Sarah Palin kabla ya kumteua kuwa makamu wake wa rais.Katika jamii ambako mwanasiasa anapaswa kueleza kila kitu- kuanzia afya hadi pato lake,habari za kushangaza si mambo yanayokaribishwa.Yaliyomkuta Palin ni matokeo ya unafiki wa maadili unaokutikana Marekani tangu miongo kadhaa."lamalizia BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG.

Gazeti la BAADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN likiendelea na mada hiyo linasema: "Kawaida masuala yanayohusika na maisha ya binafsi ya wanasiasa wa Ujerumani ni mwiko kwa vyombo vya habari,isipokuwa kama mambo hayo yanavuka mipaka ya uhalifu au habari hizo za binafsi zinachomoza wenyewe hadhrani.

Lakini nchini Marekani mambo ni tofauti kabisa:kwani huko kila kinachohusika na maisha ya binafsi ikiwa ni zuri au baya,hugonga vichwa vya habari.Ili kuweza kufanikiwa,mwanasiasa wa Kimarekani anapaswa kueleza wazi wazi mambo yake ya ndani.Makosa au dosari yoyote ya familia hulaimiwa mwanasiasa binafsi,bila ya kujali mafanikio yake ya kisiasa.Huo si mtindo mzuri,lakini hiyo ni Marekani.Na sasa ndio yamemkuta Sarah Palin binafsi.