1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAGAZETI YA UJERUMANI JUU YA PEMBE YA AFRIKA

Abdu Said Mtullya13 Agosti 2011

Pembe ya Afrika katika kurasa za mbele za magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/12G14
Wasomali wapelekewa misaada.Picha: dapd

Janga la njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika linaendelea kuzingatiwa katika kurasa za mbele za magazeti ya Ujerumani vile vile. Lakini magazeti hayo pia yanatilia maanani kwamba kwa jumla kilimo kinazidi kuwa cha ufanisi barani Afrika.

Gazeti la die tageszeitung limeinukulu wizara ya mambo ya nje ya China ikikanusha madai yaliyotolewa na mshauri wa serikali ya Ujerumani juu ya masuala ya Afrika,kwamba China inasababisha njaa barani Afrika kutokana na sera yake ya kununua ardhi ya waafrika.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha juu ya tahadhari zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa WFP Josette Sheeran ambazo hazikutiliwa maanani na jumuiya ya kimataifa. Gazeti hilo linakumbusha kwamba mkurugenzi huyo Josette Sheeran alifanya ziara kwenye eneo la pembe ya Afrika mnamo mwezi wa Aprili. Wakati huo alitahadharisha kwamba watu milioni tano tayari walikuwa wanasibika na njaa na kwamba palikuwa na hatari ya idadi hiyo kuongezeka.

Lakini hakuna alietaka kumsikiliza na tokea wakati huo idadi ya watu wanaosibika na njaa imeongezeka kwa zaidi ya milioni moja na laki nne. Mnamo mwaka 2008 Mkurugenzi huyo alishatahadharisha juu ya hatari ya kupanda bei ya vyakula muhimu kama mahindi na ngano. Aliifananisha hali hiyo na Tsunami ya kimyakimya.Athari za kupanda bei hadi asilimia 160 zimelikumba pia shirika na chakula la WFP . Dunia ilitanabahi baada ya Umoja wa Mataifa kupiga la mgambo wiki tatu zilizopita juu ya hali ya pembe ya Afrika.

Hata hivyo hali siyo ya kukatisha tamaa kabisa barani Afrika. Huo ni ujumbe wa gazeti la Die Welt. Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba licha ya maafa ya njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika, nchi nyingi barani Afrika zinaendesha sera za kilimo za ufanisi. Gazeti hilo limewakariri watalaamu wakisema kwamba siku moja bara la Afrika litakuwa na uwezo wa kulilisha bara la Asia. Gazeti la Die Welt linatilia maanani katika makala yake,kwamba katika nchi 20 za Afrika, ikiwa pamoja na Tanzania uwekezaji katika kilimo umeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Gazeti la die tageszeitung limelikunuku tamko la wizara ya mambo ya nje ya China linalokanusha madai yaliyotolewa na Mshauri wa masuala ya Afrika wa serikali ya Ujerumani, bwana Günther Nooke kwamba sera ya China ya kununua ardhi barani Afrika inasababisha maafa ya njaa katika bara hilo.

Gazeti la die tageszeitung limeeleza kwamba bwana Nooke aliyasema hayo katika mahojiano ya hivi karibuni. Gazeti hilo limeinukulu taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China ikisema kwamba China haijawahi kununua ardhi barani Afrika. Hata hivyo mshauri wa serikali ya Ujerumani juu ya masuala ya Afrika bwana Nooke ameyasahihisha matamshi yake.

Katika mahojiano na Gazeti la die tageszeitung bwana Nooke amesema kuwa China haina hatia juu ya njaa barani Afrika. Ameliambia gazeti hilo kwamba alichosema ni kuwa wote wanaonunua ardhi barani Afrika wanapaswa kufuata sera ya uwazi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limechapisha makala juu ya harakati za Eritrea nchini Somaliana katika sehemu zingine za Pembe ya Afrika. Gazeti hilo linaiita nchi hiyo kuwa mfadhili wa kimya kimya wa al-shabaab. Frankfurter Allgemeine linaarifu kuwa Kundi la al- shabaab nchini Somalia siyo la kigaidi tu, bali pia sasa linaendesha shughuli za kiuchumi. Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa kundi hilo linaingiza kati ya dola milioni 70 na Milioni 100 kwa mwaka kutokana na ushuru wa forodha na kusafirisha mkaa Saudi Arabia.

Katika makala yake gazeti la Frankfurt Allgemeine pia limearifu kwamba magaidi wa al -Shabaab wanapewa fedha na Eritrea.Kwa mujibu wa gazeti hilo wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanahoji kuwa nchi hiyo inahatarisha usalama wa eneo la Pembe ya Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba hivi karibuni nchi hiyo ilihusishwa na tuhuma za kula njama za kupanga mashambulio kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.

Mwandishi/ Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/- Josephat Charo/