1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti juu ya nishani ya amani ya Nobel

Abdu Said Mtullya11 Desemba 2012

Wahariri wanazungumzia juu ya tuzo ya amani ya Nobel iliyokabidhiwa mjini Oslo kwa Umoja wa Ulaya. Jee Umoja huo unastahiki kutunukiwa nishani hiyo?

https://p.dw.com/p/16zvS
Sherehe ya kuukabidhi Umoja wa Ulaya nishani ya amani ya Nobel mjini Oslo
Sherehe ya kuukabidhi Umoja wa Ulaya nishani ya amani ya Nobel mjini OsloPicha: Reuters

Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" anasema kuwa Umoja wa Ulaya unastahili kupewa tuzo ya amani ya Nobel. Mhariri huyo anaeleza kuwa aghalabu kamati ya Nobel imepitisha maamuzi yaliyobabisha maswali mengi lakini hapana shaka uamuzi wakuupa tuzo Umoja wa Ulaya ni sahihi kabisa.

Vita kuu mbili,maangamizi ya wayahudi,vita baridi na kugawanywa kwa bara la Ulaya.Katika muktadha huo, juhudi za kuunda Umoja wa Ulaya siyo jambo la sadfa. Bali ni matokeo ya juhudi kubwa za kudumisha amani. Ndiyo sababu Umoja wa Ulaya unapaswa kuifurahia tuzo ya amani ya Nobel.

Mhariri wa gazeti la "Rhein-Zeitung" pia anasema tuzo ya Nobel iliyotolewa kwa Umoja wa Ulaya siyo nishani tu. Ni changamoto kwa Umoja huo, na pia ni wajibu wa kuulinda na kuendeleza, mradi wa mafanikio ulionzishwa na "wazee wetu."

Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaupongeza Umoja wa Ulaya kwa kusema kwamba ufanisi wa kihistoria wa Umoja wa Ulaya unapaswa kutambuliwa. Endapo ufanisi huo usingelikuwapo,basi hadi leo Umoja wa Ulaya ungelikuwa na wanachama sita tu, badala ya 27.


Katika nyakati hizi za mgogoro mkubwa wa madeni, mshuko wa uchumi na ukosefu wa ajira,Umoja wa Ulaya unastahiki pongezi .! Hayo anayasema mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten" na anaeleza kuwa hasa sasa Umoja wa Ulaya unahitaji kuonyeshwa kwamba unakubalika.Ndiyo sababu ni sahihi kwamba Umoja wa Ulaya umetunukiwa nishani ya amani ya Nobel. Tuzo hiyo ni ishara ya ufanisi wa miaka mingi katika juhudi za kuleta maridhiano na ushirikiano.

Licha ya juhudi za Umoja wa Ulaya kutambuliwa kwa kutunukiwa nishani ya amani, Umoja huyo bado haujafikia lengo lake, yaani kuundwa kwa Umoja wa nchi za Ulaya .Hayo ni maoni ya gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung"

Na mhariri wa "Frankfurter Allgemeine" anatilia maanani hofu za baadhi ya watu juu ya Umoja wa Ulaya. Mhariri huyo anafafanua: Kwa baadhi Umoja wa Ulaya haujafanya ya kutosha juu ya haki za binadamu duniani.Wengine wanasema Umoja wa Ulaya bado haujawa nguvu kubwa ya kijeshi. Wengine wanahofia kuwa Umoja wa Ulaya sasa umo njiani kujenga urasimu utakaobana uhuru na maendeleo ya kiuchumi.

Mwandishi:Mtullya abdu.Deutsche Zeitung/

Mhariri:Yusuf Saumu