Magaidi walenga kuwashambulia raia wa kigeni nchini Algeria. | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Magaidi walenga kuwashambulia raia wa kigeni nchini Algeria.

Kila mara makundi ya Waislamu wenye imani kali, kama el-Qaeda katika mataifa ya Afrika magharibi nchini Algeria yamekuwa katika wiki za hivi karibuni yakijaribu kuonyesha nia yao ya kushambulia. Kundi hilo likiwa linajishughulisha nchini Algeria , na limekwisha tamka, kuwa linalenga kuwashambulia wageni nchini humo hususan kwa nia ya kuwaondoa raia wote wa Hispania na Ufaransa.

Ayman al-Zawahiri , aliyekuwa akishikilia nafasi ya pili katika kundi la mtandao wa kigaidi la al-Qaeda , amewatolea mwito Waislamu , katika mataifa ya maghreb kuzisafisha nchi hizo dhidi ya watu kutoka Hispania na Ufaransa. Sio ajabu basi , kwamba kwa raia wa kigeni hususan nchini Algeria , ambako pia Wajerumani wengi wanafanya kazi , hofu inazidi kupanda.

Kama kuna kitu ambacho hakina upungufu nchini Algeria ni polisi. Katika makutano kadha ya barabara na katika mitaa, wanakuwapo, lakini hisia za kuwapo kwa usalama hazipo, kama anvyosema Winfried Arpogaus. Amekuwapo nchini humo tangu miaka 20 iliyopita.

Katika miaka 2001, 2002 hali usalama hapa ilikuwa nzuri. Sijawahi kupata kuhofia.lakini hivi sasa kwa mara ya kwanza hali hiyo imenijia tangu shambulio lililopita. Hii inafanya kwa kiasi fulani mtu kujiuliza. Mtu anapaswa kuchukua tahadhari.

Kampuni anayofanyia kazi Arpogaus nchini Algeria inashughulika na jeshi la zima moto. Kwa hiyo ni lazima asafiri katika maeneo mengine nchini humo. Mara nyingine husafiri kwa ndege. Kusafiri kwa gari imekuwa jambo la hatari sana. Hofu imekuwa kubwa mno kwa kutokea hatari ya mashambulizi , na mabomu ya kujitoa muhanga.

Watu 111 wameuwawa katika muda wa nusu mwaka uliopita. Shambulio la hivi karibuni kabisa lilifanyika tarehe 21 Septemba wakati bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara lilipolipuka karibu na mlolongo wa magari ya raia wa kigeni. Watu tisa walijeruhiwa na miongoni mwao raia watatu kutoka Ulaya. Shambulio moja linafuatiwa na jingine na ndio sababu hali ni ya tahadhari sana. Karim ambaye ni dereva nchini Algeria anafafanua.

Kuna amri iliyotolewa kuwa hatupaswi kufuata njia moja tu kila siku. Na wakati huo tunatakiwa tuwe kimya. Wakati tunaendesha , tunasindikizwa na magari ya polisi. Na kuna njia ambazo tunatakiwa kutopita kabisa.

Karim hataki kutaja jina lake kamili, na ni watu wangapi ambao nchini Algeria wanabaki kimya kuhusu mada kama hizi. Wana hofu , kwamba dhana ya ukuaji wa uchumi nchini Algeria inaweza kuharibika. Kwamba wafanyakazi wa makampuni ya kigeni wanaweza kuondoka na mikataba mingi minono inaweza kufutwa. Raia wa kigeni wapatao 32,000 wanafanyakazi rasmi nchini humo, wakiwa wengi wao ni Wachina, wajerumani na Wafaransa. Kwa upande wa watu kutoka Ulaya, Wafaransa wamewekeza fedha nyingi sana hapa. Na kutokana na historia ya ukoloni kwa nchi hiyo Ufaransa imekuwa ikichukiwa zaidi na Waislamu wenye imani kali. Mtaalamu wa masuala ya kigaidi Mathieu Guidere ambaye pia ni profesa katika chuo kikuu cha Genf anasema.

Nchini Algeria wawekezaji wa Kifaransa wanafanyiwa bughudha wasirejee na kurejesha uhusiano wa kiuchumi na serikali ya Ufaransa. Hali hii imeletwa na kiongozi namba mbili wa al – Qaeda katika mataifa ya maghreb, baada ya kutoa wito kwa Walgeria kupambana na Wafaransa.

Na dhidi ya Wahispania , magaidi wanapambana nao , hususan kutokana na maeneo mawili yanayomilikiwa na Hispania katika ardhi ya Morocco. Guidere anawaonya raia wa kigeni kujiweka katika maeneo ya usalama. Anaonya Guidere kwamba lengo la El-Qaeda ni kuwafukuza raia wote wa kigeni kutoka mataifa ya Afrika kaskazini. Hapa hakuna tofauti baina ya Mfaransa ama Mjerumani.

 • Tarehe 02.10.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7M
 • Tarehe 02.10.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7M

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com