1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magaidi 20 wauliwa Sinai

Abdu Said Mtullya8 Agosti 2012

Wanajeshi wa Misri wamewaua watu 20 wanaotuhumiwa kuwa waislamu wenye itikadi kali katika eneo la Sinai linalopakana na Israel. Helikopta za jeshi la Misri ziliwashambulia watu hao kwa makombora.

https://p.dw.com/p/15lgt
Mpaka baina ya Israel na Misri,Sinai
Mpaka baina ya Israel na Misri,SinaiPicha: Reuters

Israel imewapongeza wanajeshi wa Misri kwa kuwakabili wapiganaji wa kiislamu wenye itikadi kali katika eneo la Sinai, katika juhudi za kuwasaka watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya wanajeshi 16 wa Misri mwishoni mwa wiki iliyopita. Afisa mwandamizi kattika wizara ya ulinzi nchini Israel Amos Gilad amesema Misri ndiyo yenye mamlaka juu ya eneo la Sinai na nchi hiyo itafanya kila linalopasa katika uwezo wake ili kuwakabili magaidi. Afisa huyo amesema mafanikio ya Misri yatakuwa na maana ya kuyazuia mashambulio makubwa zaidi

Mashambulio ya jeshi la Misri ambayo ni ya kwanza katika eneo la Sinai baada ya miaka mingi, yalifanyika katika kijiji cha Tumah wakati majeshi ya usalama yaliwekwa tayari karibu na kivuko cha Rafah kwenye mpaka baina ya Misri na Ukanda wa Gaza.

Afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Misri katika eneo la Sinai aliezungumza na waandishi wa habari bila ya kulitaja jina lake aliarifu kwamba magaidi 20 waliuawa kutokana na shambulio lililofanywa na helikopta wakati askari wa miguu walipoingia katika kijiji cha Tumah. Afisa huyo ameeleza kuwa majeshi ya Misri bado yanaendelea na operesheni ya kuwasaka magaidi.

Maafisa wengine wa usalama wa Misri wamearifu kwamba ndege za kijeshi za Misri zilifanya mashambulio katika mji wa Sheikh Zuwayid karibu na kijiji cha Tumah. Maafisa hao wamesema kuwa watu wasiojulikana walivishambulia vituo vinne vya udhibiti wa usalama karibu na mji wa El- Arish.

Majeshi ya Misri yamefanya mashambulio hayo siku moja baada ya maziko ya askari 16 wa Misri waliouawa mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la Sinai. Askari hao waliuawa baada ya magaidi kuyatwaa magari mawili ya deraya na kuvuka nayo, mpaka wa Israel. Gari moja lililokuwa limejaa mabomu liliripuka, na jingine lilikatizwa safari baada ya kushambuliwa na ndege ya Israel.

Gazeti la serikali ya Misri Al-Ahram liliarifu juu ya kuendelea kwa mapambano kwenye vituo vya udhibiti wa usalama katika mji wa El Arish baada ya majeshi ya usalama kuyazima mashambulio ya awali katika vitongoji vya mji huo. Habari zaidi zinasema kuwa majeshi ya Misri yanaendelea kuwasaka magaidi, baada ya kuingia katika sehemu za milimani, kusini mwa mji wa El- Arish.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afpe

Mhariri: Miraji Othman