1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yauwa watu 48 Saudi Arabia

Mohamed Dahman26 Novemba 2009

Watu arobaini na nane wamefariki katika mji wa bandari wa Saudi Arabia wa Jeddah kufuatia kunyesha kwa mvua kubwa sana kuwahi kushudiwa nchini humo katika miaka mingi.

https://p.dw.com/p/Kgnb
Mahujaji wa Kiislamu wakiwa katika Mlima Arafat nchini Saudi Arabia Alhamisi tarehe 26 Nov. 2009 kukamilisha ibada ya hija.Picha: AP

Baadhi ya watu wamekufa maji wengine wamekufa kutokana na kuanguka kwa madaraja na kutokana na ajali za magari.Ibada ya hija inayofanyika katika mji mtakatifu wa Mecca nchini Saudi Arabia imetibuliwa na mvua hiyo kubw

Watu 900 wameokolewa baada ya kukwama kutokana na maji ya mafuriko yaliosababishwa na mvua hiyo kubwa ya hadi inchi 3 sawa na centimita 76.Idadi ya vifo katika mji wa Jeddah imefikia watu 44 wakati watu wengine wanne wamekufa katika jimbo la Mecca. Takriban watu milioni moja na laki sita kutoka nchi za nje wamekwenda Saudi Arabia kutimiza ibada hiyo ya Hija ambao ni mkusanyiko mkubwa wa kidini wa kila mwaka duniani lakini hakuna alieripotiwa kuwa miongoni mwa wahanga hao wa mafuriko.

Hata hivyo mafuriko hayo yamelazimisha kufungwa kwa barabara kuu kuelekea katika mji wa Mecca na hiyo kukwamisha mahujaji ambao hapo jana walishindwa kukamilisha safari yao.Mvua hiyo ambayo sio ya kawada katika taifa hilo la kifalme la jangwa imefurika njia na majengo mjini Jeddah ambapo ni kituo kikuu cha kuingilia mahujaji nchini Saudi Arabia.

Baadhi ya mahujaji milioni 2. 5 wa Kiislamu walisema wangeliacha kwenda kukesha katika bonde la Mina hapo jana usiku kwa sababu mvua hiyo imevuruga huduma za usafiri wa mabasi kutoka Mecca.Badala yake walitazamiwa kubakia katika mji mtakatifu wa Mecca na asubuhi hii kuelekea moja kwa moja katika Mlima Arafat ambapo Mtume Muhammad SAW alitowa risala yake ya mwisho na ambapo mahujaji wanatakiwa kusoma Koran na kuomba Mungu.

Mapema hapo jana mvua hiyo ilizusha wasi wasi miongoni mwa maafisa wa hija na mahujaji wanotekeleza ibada hiyo kwamba ingelisababisha mafuriko.Mamia ya mahujaji walikuwa wamekwama kwenye mabasi katika barabara ya kilomuita 80 kutoka Jeddah kuelekea Mecca.Maelfu kwa maelfu ya mahujai wengine walijitosa mvuani kuelekea Mina ilioko kilomita tano kutoka Mecca lakini wengine walikwama wakati wakijaribu kutumia mabasi.Umeme ulikatika katika baadhi ya sehemu za mji wa Mecca. Medina na Jeddah kwa sababu ya dhoruba hiyo ya mvua.

Mkururo wa mahujaji kutoka duniani kote walianza ibada hiyo ya siku tano ya hija hapo Jumanne na mapema Jumatano wakilizunguka Kaaba ndani ya msikiti mkuu wa Mecca.Ibada ya hija inatakiwa kutekelezwa na kila Muislamu mwenye uwezo na afya angalau mara moja katika maisha yake.

Wasaudi walikuwa wakitarajia kupokea wageni milioni mbili mwaka huu kwa ajili ya ibada hiyo ya hija.Lakini idadi ya mahujaji ndani ya nchi hiyo waliokadiriwa kufikia karibu milioni moja mwaka jana wanatarajiwa kupungua sana kwa sababu ya hofu ya homa ya mafua ya nguruwe.


Mwandishi:Mohamed Dahman /AFP

Mhariri:Abdul-Rahman