1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafaili ya hati ya kusafiria ya Obama yachunguzwa

Charo, Josephat21 Machi 2008

Wafanyakazi wawili wa muda wa wizara ya mambo ya ndani wafutwa kazi

https://p.dw.com/p/DSFD
Seneta wa jimbo la Illinois Barack ObamaPicha: AP

Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani imewafuta kazi wafanyakazi wake wawili wa muda kwa kuchunguza mafaili ya pasi ya kusafiria ya mgombea uteuzi wa kuwania urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, seneta Barack Obama. Wakati huo huo, gavana wa jimbo la New Mexico, amemuunga mkono Barack Obama ateuliwe kugombea urais wa Marekani.

Kampeni ya chama cha Democratic ya kuwania kuingia ikulu ya Marekani imekabiliwa na utata huku kukiwa na taarifa kwamba watumishi wawili wa muda wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, walichunguza mafaili ya hati ya kusafiria ya seneta wa jimbo la Illinois, Barack Obama.

Msemaji wa wizara hiyo, Sean McCormack, amesema hatua ya haraka imechukuliwa na ameapa kuwa uchunguzi wa kina utafanywa. Ameieleza hatua ya wafanyakazi hao kuchunguza faili za Obama kuwa isiyo ya busara na ya kijinga.

Timu ya kampeni ya seneta Obama imeulaumu utawala wa rais Geroge W Bush kwa kitendo hicho cha ufisadi kinachopinga kabisa maadili na kuikiuka haki ya kibinafsi ya kutoingiliwa kwa masilahi ya kisiasa.

Seneta Obama, ambaye anakabiliana na seneta Hillary Clinton, katika mashindano makali ya kuwania uteuzi wa chama cha Democratic kuweza kugombea urais wa Marekani mwezi Novemba mwaka huu, ametoa taarifa kali akiuonya utawala wa rais Bush kwa kutojali kikamilifu haki za wamarekani.

Msemaji mwingine wa wizara ya ndani ya Marekani, Pat Kennedy, amethibitisha wafanyakazi wawili wamefutwa kazi na mwingine wa tatu kuadhibiwa. Hata hivyo msemaji huyo hakutoa maelezo yoyote kuhusu aina ya habari zilizopatikana kwenye mafaili ya pasi ya kusafiria ya seneta Obama.

Msemaji huyo pia amekataa kuwataja wafanyakazi waliofanya uchunguzi huo wala kuitaja mifungamano yao ya kisiasa akiongeza kuwa visa vya uchunguzi wa mafaili ya Obama vilifanywa wakati tofauti mnamo mwezi Januari, Februari na mwezi huu. Hata hivyo amethibitisha kwamba hatua za haraka zimechukuliwa kuhakikisha ikiwa uchunguzi huo una nia yoyote dhidi ya seneta Obama.

Maafisa wa wizara ya ndani ya Marekani wanatarajiwa hii leo kukutana na maafisa wa kampeni ya Obama kulijadili swala hilo. Msemaji wa seneta Obama, Bill Burton, amesema swala hilo linahitaji kuchunguzwa kwa kina na wanataka kujua ni nani aliyeichunguza faili ya pasi ya kusafiria ya Seneta Obama, kwa lengo gani na kwa nini imechukua muda mrefu kwa wizara ya mambo ya ndani kutangaza ukiukaji huo wa usalama.

Obama aungwa mkono na gavaya wa New Mexico

Wakati haya yakiarifiwa, gavana wa jimbo la New Mexico, Bill Richardson, amemuunga mkono Barack Obama kuwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic. Kesho gavana huyo anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa hadhara wa Obama huko Portland.

Barack Obama na Hillary Clinton wamekuwa wakiwania kuungwa mkono na gavana Richardson kwa kuwa ni mmarekani mwenye nasaba ya kihispania na anaonekana kuwa mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa jamii ya Walatino nchini Marekani, ambao huenda wakachangia sana katika kuamua matokeo ya uchaguzi wa urais hapo mwezi Novemba.

Wapigaji kura wa kilatino wameongezeka kwa kasi kubwa na kuwa sehemu muhimu ya wapiga kura wa Marekani. Walimuunga mkono Hillary Clinton wakati wa uchaguzi wa awali uliojulikana kama Supper Tuesday. Lakini hatua ya gavana wa jimbo la New Mexico kumuunga mkono Obama, huenda ikabadili msimamo wa jamii hiyo wakati wa uchaguzi mkuu.