1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Poland kupinga sheria tata

Bruce Amani
21 Julai 2017

Maelfu ya Wapoland wamefanya maandamano usiku kucha kupinga sheria mpya ambayo inaliruhusu bunge kuwateua majaji wa Mahakama ya Juu, hatua inayokiuka onyo la Umoja wa Ulaya kuwa inahujumu demokrasia na mkondo wa sheria.

https://p.dw.com/p/2gvoa
Polen Protest gegen Justizreform in Warschau
Picha: Reuters/Agencja Gazeta/A. Grzybowska

Mswada huo, ambao uliwasilishwa na chama tawala cha Sheria na Haki - PiS, ulipitishwa na bunge mapema jana baada ya mjadala mkali. Hali hiyo ilizusha mojawapo ya maandamano makubwa kabisa tangu chama hicho kilipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka wa 2015.

Kura hiyo ilipigwa siku moja baada ya Umoja wa Ulaya kumpa mwanachama wake huyo muda wa wiki moja kuachana na mabadiliko hayo ambayo umoja huo unasema unaziweka mahakama chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa serikali.

Kama chama cha kizalendo cha PiS nchini Poland hakitasikia wito huo, serikali huenda ikakabiliwa na faini na hata kunyimwa haki za kupiga kura, ijapokuwa nchi nyingine zinazouangalia Umoja wa Ulaya kwa jicho la pili kama vile Hungary, zinaweza kuzuia kupitia kura ya turufu vikwazo vikali dhidi ya Poland. GRZEGORZ SCHETYNA ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Civic Platform "mtu anayeishi katika Ikulu hii nyuma yetu, ana nafasi nzuri ya kuonyesha kuwa yeye ni rais wa Wapoland wote. anahitaji tu kufanya kitu kimoja. kupinga miswada mitatu. na leo tunamwambia aipinge miswada hiyo"

Polen Parlament in Warschau, Debatte Justizreform
Mswada huo ulizusha majadala mkali bungeniPicha: Reuters/Agencja Gazeta/S. Kaminski

Serikali inasema mabadiliko hayo yanahutajika ili kuzifanya mahakama kuwajibika zaidi na kuhakikisha taasisi za serikali zinawahudumia Wapoland wote na sio tu wa "tabaka la juu” ambao inasema ndio wanaounga mkono upinzani wa msimamo wa wastani. Waziri Mkuu Beata Szydlo anasema hawataruhusu mataifa ya nje kuingilia maswala yao ya ndani "Tuna maono ya mabadiliko. ndio maana kazi yetu ni ya haraka na ya uhakika. Hatutaangushwa na shinikizo. Hatutaruhusu watu watetezi wa kigeni wa wasomi wa Poland kututisha. Chama cha Sheria na Haki kilishiriki uchaguzi na mpango wa kuufufua uchumi wa nchi yetu".

Mswada huo utajadiliwa leo katika baraza la Seneti ambako chama cha PiS kina wingi mkubwa wa viti. Duda, ambaye ni mshirika wa chama hicho, atahitajika kuusaini mswada huo kabla ya kuwa sheria.

Wakosoaji ndani na nje ya nchi wanasema sheria hiyo ni sehemu ya mchakato wa kuelekea katika utawala wa ubabe, ambao unajumuisha siasa za kizalendo pamoja na sera za kiuchumi zinazoegemea siasa  za mrengo wa kushoto. Nao wapinzani wa kisiasa, makundi ya kutetea haki na Umoja wa Ulaya wanasema mabadiliko hayo yanahujumu mgawanyo wa madaraka kati ya ofisi ya rais na idara ya mahakama, ambao ni msingi muhimu wa kidemokrasia.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo