1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maduka ya kiafrika Ujerumani yakumbwa na hofu

Aboubakary Jumaa Liongo9 Juni 2010

Madhara ya kuyumba kwa sarafu ya Euro yanaonekana karibu kila mahali, hususan kwa wafanya biashara wanaoingiza bidhaa za vyakula katika nchi zinazotumia sarafu hiyo ya Euro.

https://p.dw.com/p/NmND

Tokea mwishoni mwa mwaka jana, thamani ya Euro dhidi ya Dola imeshuka thamani kwa asilimia 20 na hali hiyo imeendelea kuwa hivyo. Na gharama za kuagiza bidhaa hizo nazo pia zimepanda. Zaidi hasa hali hiyo imewakumba wafanya bishara wadogowadogo, ambao hawana mitaji mikubwa, na ambao pia hawawezi kupata mikopo kutoka mabenki.

Rebecca Saprong Aboagye ni mfanyabishara kutoka Ghana ambaye ana duka katikati ya jiji la Cologne nchini Ujerumani linalouza bidhaa za kiafrika, liitwalo Becky Afroshop. Anaagiza na kuuza bidhaa za kiafrika, hususan vyakula kama vile ndizi, viazi, Bilinganyi na Samaki wakavu.

Kuyumba kwa sarafu ya Euro kumeifanya biashara yake mwezi hata mwezi kuwa ngumu zaidi, na anasema

´´Huwa ninatuma fedha (Euro) Ghana, ili waweze kuninunulia bidhaa na kunitumia. Lakini tokea sarafu ya Euro ilipoyumba, hivi sasa siwezi kuagiza bidhaa hizo, kwasababu nikipiga mahesabu, kama nikinunua, nitaziuza vipi, naona nitapata hasara. Kwa kweli nimesitisha kabisa kuagiza bidhaa´´

Kutokana na hali hiyo, upatikanaji wa bidhaa hizo katika duka la Rebecca umekuwa mgumu. Mfano samaki wakavu kwa sasa hawako tena. Kwa kawaida, maboksi yaliyojaa viazi vitamu huwa tele katika meza za duka hilo, lakini sasa kilichoko ni vitunguu tu.

Iwapo bidhaa hizo za vyakula zingeagizwa, gharama itakuwa kubwa , kwa hivyo pia vitalazimika kuuzwa kwa bei ghali.

Lakini kwa Rebecca Sarpong Aboagye, suala si kupandishwa kwa bei, bali ni wasiwasi wa kupoteza wateja.

Ili kujikwamua kutoka katika kizungumkuti hiki, anapanga kupitisha ushauri muhimu hivi karibuni, na kuongeza.

´´Kwa kweli nimejipa muda, ni suala la kusubiri, nimejipa muda wa kama miezi miwili hivi au mitatu kuangalia iwapo hali itaweza kubadilika au labda miujiza inaweza kutokea kusikojulikana. Kama hali itaendelea kubakia hivyo, hivyo basi sina budi nitafunga biashara hii na kufungua biashara nyingine, kwa sababu huwezi kuendelea katika mazingira ya hali kama ilivyo hivi sasa´´

Kwa wateja kununua vyakula vya kiafrika, kunatoa nafasi pia kwa fedha kupelekwa katika nchi kama vile Ghana, Togo au India.

Wahamiaji wengi hapa Ujerumani husaidia familia zao, jamaa na marafiki huko makwao, kwa kuwatumia fedha.

Benki ya dunia imesema kuwa zaidi ya dola millioni 300 zimekuwa zikitumwa kila mwaka katika nchi zinazoendelea. Kiwango hiki ni kikubwa kuliko misaada ya maendeleo inayotolewa kwa nchi hizo.

Kwa nchi masikini, kama vile Ghana, inategemea sana fedha zinazotumwa na wananchi wa nchi hiyo waliyoko nje, kama chanzo chake muhimu cha mapato. Mwaka 2008, kwa mujibu wa takwimu za benki kuu ya nchi hiyo, takriban dola millioni tisa zilitumwa nchini humo na watu binafsi au taasisi zisizo za kiserikali waliyoko nje.

Wakati ambapo mfanya biashara huyo wa Ghana akisubiri kuimarika tena kwa sarafu ya Euro, ndugu zake wengi waliyoko Afrika wanajiuliza zimekwenda wapi fedha walizokuwa wakipata . Wanategemea msaada wa fedha kutoka Ulaya na pia wanaangalia kwa wasi wasi taarifa za kila siku katika maduka ya kubadilishia fedha jinsi thamani ya Euro inavyoshuka.

Mwandishi:Mohammad Awal/Aboubakary Liongo

Mhariri:Othman Miraji