1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madereva wa treni wagoma nchini Ujerumani

Tuma Provian Dandi12 Oktoba 2007

Wakazi wa Ujerumani waotumia usafiri wa treni kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika miji mikubwa wamekumbwa na tatizo la usafiri kufuatia mgomo wa madereva

https://p.dw.com/p/C7hs
Abiria wa Ujerumani wakisubiri usafiri
Abiria wa Ujerumani wakisubiri usafiriPicha: AP

Zaidi ya nusu ya treni zinazosafirisha abira kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine na zile za safari fupi katika miji mikubwa nchini Ujerumani, hazikuwa zikifanya kazi kutokana na mgomo wa madereva wanaoitaka serikali kuwaongezea mishahara na maslahi mengine.

Mkurugenzi wa shirika la reli la Ujerumani-Deustche Bahn Karl Friedrich Rausch ameviambia vyombo vya habari kwamba hali ilikuwa ngumu zaidi katika miji ya Munich, Stuttgart na Berlin ambapo wasafiri wamepata usumbufu mkubwa ikiwemo kuchelewa kwenda kazini au kwenye shughuli nyingine.

Ofisa huyo wa shirikal la reli la ujerumani amesema mgomo huo umesababisha hasara kubwa, na kwamba hakuamini kuwa ungetokea hadi alipoona treni hazifanyi kazi.

Mjini Munich ni treni zinazotoka katikati ya mji kwenda kwenye kiwanja cha pekee zilizokuwa zikifanya kazi.

Kampuni ya ADAC inayojihusisha na masuala ya usafiri wa magari imesema leo barabara nyingi zilikuwa na foleni ya magari mengi kutokana na mgomo wa madereva wa treni za kusafirisha abiria.

Mgomo huo pia umesababisha kero kwa wanafunzi wa shule na vyuo katika majimbo sita ya Ujerumani, ambao leo hii walikuwa wakianza likizo zao.

Kwenye kituo kikuu cha treni mjini Frankfurt, maofisa wa shirika la reli la Ujerumani na madereva wao wameonekana wakinywa kahawa na vinyjwaji vingine bila kujali wala kuwa na hofu kwamba wanavuruga ratiba na majukumu ya wananchi.

Jumuiya ya wafanyakazi wa shirila la reli la Ujerumani, wamesikika wakiiambia serikali kwamba wanataka maslahi yao yazingatiwe kwa vile wanalipwa kiasi kichowaridhisha ikizingatiwa kwamba kazi yao ni ngumu.

Madereva hao wametangaza muda wa saa 22 za kutofanya kazi hadi pale mahitaji yao yatakapozingatiwa na serikali ikiwemo kushughulikiwa mikataba yao.

Kila inapotokea kwamba wafanyakazi wa ujerumani wanataka kutimiziwa mahitaji yako ikiwemo mishahara na mazingira mazuri ya kazi, vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikiungana pamoja hadi mafanikio yanapopatikana.

Juma lililopita mahakama ya Ujerumani ilitoa agizo la kutofanya mgomo huo kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kuathiri uchumi wa nchini na kwamba madai ya wafanyakazi wa shirika la reli yangefikia ufumbuzi.

Madereva hao wa treni za mijini na nje ya mikoa wanataka nyongeza ya asilimia 31 kwenye mishahara yao pamoja na mikataba mingine kwa wafanyakazi wa shirika la reli.