1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madeni ya Marekani bado kitisho kwa uchumi duniani

2 Agosti 2011

Marekani leo inatazamiwa kujiepusha na janga la kiuchumi, wakati baraza la Seneti na Rais Barack Obama wakitazamiwa kuidhinisha makubaliano ya kupunguza nakisi ya bajeti, yaliyopatikana baada ya mijadala mikali.

https://p.dw.com/p/RdZw
With a week remaining before the national vote, the Capitol is seen in Washington, Tuesday, Oct. 26, 2010. President Obama and his Democrat majority in Congress could become victims of voter anger over the economy, likely to give Republicans control of the House of Representatives, and considerably diminish their Senate majority. (AP Photo/J. Scott Applewhite)
Bunge la Marekani mjini WashingtonPicha: AP

Seneti ya Marekani inayodhibitiwa na chama cha Demokratic inatazamiwa kuidhinisha mswada uliopitishwa na Baraza la Waakilishi, linaloongozwa na chama cha Republican licha ya kupingwa vikali na wanachama wote wawili wa kihafidhina wa Tea Party na wanachama wa Demokratic wenye sera za wastani walioghadhibishwa na uwezekano wa kuathirika miradi ya kuwasaidia masikini. Hata hivyo, mswada huo unatazamiwa kuidhinishwa na Seneti baadae leo hii na muda mfupi baadae utakuwa sheria baada ya kutiwa saini na Rais Obama.

Hatua hiyo itaashiria mwisho wa mivutano kati ya vyama vya Democratic na Republican iliyoikwamisha serikali ya Marekani kwa majuma kadhaa. Mivutano hiyo pia imezusha hofu miongoni mwa wawekezaji, ambao tayari wana wasiwasi kuhusu uchumi dhaifu wa Marekani pamoja na matatizo ya madeni yanayokabiliwa na baadhi ya serikali barani Ulaya.

President Barack Obama delivers a statement to members of the media at the North Atlantic Council summit in Lisbon , Portugal, Friday, Nov. 19, 2010. (AP Photo/Pablo Martinez Monsivais)
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Masoko ya fedha yalipumua kufuatia maafikiano ya Jumatatu lakini midahalo kuhusu nakisi ya bajeti ya serikali ya Marekani imefichua tofauti kubwa za kisiasa zinazokutikana nchini humo. Kwa hivyo, maafikiano hayo hayatoshi kuondoa kitisho cha Marekani kushushwa katika orodha ya mashirika makuu ya Marekani yanayotathmini uwezo wa serikali kulipa madeni yake. Mtaalamu wa masualu ya kiuchumi, Greg McBride amesema, azimio la kupandisha kiwango cha serikali kuweza kukopa, limeondoa hofu ya kushindwa kulipa madeni lakini halikubadili hali halisi ya kiuchumi.

Wakati huo huo, gazeti la China, People´s Daily, linaamini kuwa matatizo ya deni la Marekani bado ni kitisho kwa uchumi duniani, licha ya maafikiano yaliopatikana. Linasema, Marekani imenusurika kushindwa kulipa madeni yake, lakini matatizo ya deni bado hayakupatiwa ufumbuzi. Matamshi kama hayo katika gazeti rasmi la China si lazima kuwa ni maoni ya viongozi wa nchi hiyo.

Lakini matamshi hayo ya tahadhari,yanafanana na maoni ya serikali ya China iliyokosoa hivi karibuni katika vyombo rasmi vya habari. Kwani, China kama mkopeshaji mkubwa kabisa wa Marekani, ina wasiwasi na mali yake. Inatathminiwa kuwa asilimia 70 ya akiba yake ya fedha za kigeni ya dola trilioni 3.2 imewekezwa Marekani. Mara kwa mara, China yenye akiba kubwa kabisa ya fedha za kigeni duniani, imeihimiza Marekani kuilinda mali yake.

Mswada uliokubaliwa na Wademokrat na Warepublican haukuridhisha pande zote mbili, lakini unatazamwa kama ni ushindi kwa kambi ya Tea Party katika chama cha Republikan, iliyopinga kuongeza kodi na iliyoshinikiza kupunguza matumizi ya serikali.

Mwandishi:Martin,Prema/rtre

Mhariri:Abdul-Rahman Mohammed