1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari washambuliwa kwa kuhudumia majeruhi

21 Desemba 2011

Madaktari na wasaidizi waliojitolea, wamefungua vituo vya kutoa matibabu ya dharura kwenye uwanja wa Tahrir katikati ya mji mkuu wa Misri, Cairo kama ilivyokuwa wakati wa mapinduzi ya nchi hiyo mapema mwaka huu.

https://p.dw.com/p/13Wtl
Egyptian protesters run as they are chased by army soldiers over the Asr el-Nile bridge leading out of Tahrir Square, in Cairo, Egypt, Saturday, Dec. 17, 2011. Hundreds of Egyptian soldiers swept into Cairo's Tahrir Square on Saturday, chasing protesters and beating them to the ground with sticks and tossing journalists' TV cameras off of balconies in the second day of a violent crackdown on anti-military protesters that has left eight dead and hundreds injured. (Foto:Nasser Nasser/AP/dapd)
Vikosi vya usalama vyatumia nguvu dhidi ya waandamanajiPicha: dapd

Watu wanaojeruhiwa katika machafuko yaliyozuka upya, wanahudumiwa katika zahanati hizo za dharura na hilo ni jambo linalowakera wanajeshi. Amani Massoud ni mwanaharakati anaefanyakazi pamoja na shirika la haki za binadamu nchini Misri. Yeye huwasiliana na madaktari wanaosaidia kwenye uwanja wa Tahrir na huandika kila kitu kinachotokea huko kama anavyoelezwa na madaktari. Lakini, ripoti za madaktari na hata mashahidi, zinatofautiana kabisa na taarifa zinazotolewa na wizara ya afya.

Kwa mfano hadi Jumanne mchana, wizara hiyo iliripoti majeruhi kadhaa na hali daktari mmoja kutoka uwanja wa Tahrir siku hiyo hiyo, aliarifu kuwa tangu mapema asubuhi, zahanati ilipokea maiti nne. Hayo yalithibitishwa na madaktari wengine pia. Maiti hizo zilikuwa na alama za risasi. Waandamanaji waliokusanyika kwenye uwanja wa Tahrir walishambuliwa na wanajeshi mapema asubuhi.

Mwanaharakati Amani Massoud anasema, baraza la kijeshi,linajaribu kuficha ukatili unaotendwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji. Anasema hata madaktari na wasaidizi wanashambuliwa. Kwa mfano, msaidizi mmoja alipigwa vibaya na wanajeshi katika zahanati moja ndani ya kanisa.

"Kijana Islam, wala si daktari bali ni msaidizi, lakini alikuwa na vazi jeupe kama daktari. Mara akavamiwa na wanajeshi walioanza kumpiga marungu na mateke ya usoni huku akibururwa na akikaripiwa kwa kuwasaidia majeruhi."

Ägyptische Demonstranten auf dem Tahrir Platz in Kairo Autor: DW/Hebatallah Ismail Hafez Dezember 2011
Baraza la Kijeshi lashinikizwa kuikabidhi madaraka serikali ya kiraia

Akilalamika, mwanaharakati huyo anasema, tukio hilo ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na Katiba ya Geneva, kwani madaktari na wasaidizi lazima waruhusiwe kusaidia bila ya vitisho. Hiyo huheshimiwa hata wakati wa vita, lakini sio na baraza la kijeshi la Misri. Mwanaharakati Amani Massoud anasema kinachosikitisha ni kuwa baraza la kijeshi linaamini kuwa litaweza kujitoa kimaso maso. Lakini, katika enzi ya sasa, ulimwengu mzima unaweza kuona moja kwa moja kile kinachotokea nchini Misri.


Mwandishi: Wegerhoff, Cornelia/ZPR
Tafsiri: Martin,Prema
Mhariri:Josephat Charo