1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madagascar

Halima Nyanza28 Januari 2009

Rais wa Madagascar Marc Ravalomanana leo amemlaumu mpinzani wake kuu kwa kuendelea kuchochea ghasia za kisiasa katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo, ambazo zimesababisdha mpaka sasa vifo vya watu 34.

https://p.dw.com/p/Gi1p
Kituo cha taifa cha Televisheni nchini Madagascar kikiteketea kwa moto, baada ya kuchomwa na waandamanaji wenye hasira.Picha: AP

Maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo yaliyoitishwa na meya wa mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo, Andry Rajoelina siku ya Jumatatu, yaligeuka kuwa ghasia, baada waandamanaji hao kuiba na kuchoma moto majengo ya kituo cha taifa cha radio pamoja na kuvamia na kupora katika televisheni binafsi ya Rais wa nchi hiyo Marc Ravalomanana.


Meya Andry Rajoelina mwenye umri wa miaka 34, ambaye anamuelezea Rais Ravalomanana kuwa ni dikteta, alitangaza kusimamishwa kwa muda, lakini leo maelfu ya waandamanaji walijitokeza katika maziko ya kijana aliyeuawa katika maandamano ya Jumatatu .


Kijana huyo alipigwa risasi kichwani na walinzi mbele ya kituo cha Televisheni binafsi cha Rais Ravalomanana, ambacho pamoja na majengo ya radio ya serikali yalivamiwa na kundi hilo la watu wenye hasira.


Msaidizi wa Meya huyo wa Antananarivo awali aliarifu kuwa aliarifu kuwa kutakuwa na maandamano mapya, lakini umati wa watu waliokusanyika katika kwa ajili ya maandamano hayo waliondoka kwa amani.


Jana Kikosi cha Wafanyakazi wa kuzima moto walizigundua maiti 25 kwenye mabaki ya eneo moja la maduka yaliyoteketezwa kwa moto wakati wa ghasia hizo, miili mingine sita ilipatikana katika ghala, linalomilikiwa na Rais Ravalomanana.


Akizungumza baada ya kutembelea majengo ya radio ya serikali yaliyoharibiwa, Rais Ravalomanana amemlaumu meya wa mji huo kwa kusababisha hayo yote, na kuongeza kuwa alizuia jeshi kutoingilia katika mzozo huo kutokana na kwamba ingesababisha machafuko ya umwagaji damu zaidi.


Rais Ravalomanana ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2001, ametoa wito wa umoja wa kitaifa na mazungumzo na mpinzani wake, lakini hadi sasa viongozi hao bado hawajakutana.


Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Ufaransa Bernard Kouchner ameelezea kusikitishwa kwake na ghasia hizo zilizotokea nchini Madagascar na ametoa wito wa kuonesha uvumilivu na kukutana kwa mazungumzo pande hizo zinazopingana.


Mzozo huo uliibuka baada ya kituo cha televisheni cha Meya Rajoliena kutangaza mahojiano na rais wa zamani Didier Ratsiraka anayeishi uhamishoni nchini Ufaransa.