1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Putin wajadili makubaliano ya nyuklia ya Iran

Caro Robi
24 Mei 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakutana na Rais Vladimir Putin kujaribu kuyanusuru makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran baada ya Marekani kujiondoa kutoka makubaliano hayo ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/2yH2o
Deutschland, Hamburg, G 20, Macron und Putin
Picha: Reuters/I. Langsdon

Baada ya kushindwa kumshawishi Rais wa Marekani Donald Trump kutoiondoa nchi yake kutoka makubaliano ya kinyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu zaidi duniani mnamo mwaka 2015, Rais Macron sasa anamgeukia rais wa Urusi kutafuta njia za kuyadumisha makubaliano hayo baada ya Trump kuiondoa Marekani mapema mwezi huu.

Macron atafanya mazungumzo na Putin kuhusu suala hilo la Iran licha ya kuwepo tofauti kubwa kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Urusi kuhusu masuala mbali mbali ya kimataifa kuanzia mzozo wa Syria, wa Ukraine na madai ya Urusi kuingilia chaguzi.

Nchi za Ulaya kuyanusuru makubaliano ya Iran?

Lakini viongozi hao wawili wote wanasemekana kuwa na ari ya kuyanusuru makubaliano kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo, Urusi, China, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Marekani kudhibiti shughuli za kinyuklia za Iran na badala yake nchi hiyo ilegezewe vikwazo vya kiuchumi.

China | Bundeskanzlerin Merkel mit chinesischem Ministerpräsidenten Li Keqiang
Waziri mkuu wa China Li Keqiang na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Macron na Putin watajadiliana pia uhusiano wa kiuchumi licha ya vikwazo dhidi ya urusi vilivyowekwa baada ya kuinyakua rasi ya Crimea.

Na suala hilo la Iran ndiyo mara ya kwanza Urusi, Ufaransa na Ujerumani zinakuwa na msimamo mmoja kuhusu suala lenye uzito wa namna hiyo katika safu ya kimataifa katika kipindi cha miaka kadhaa sasa.

Aidha leo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa China Li Keqiang wameyatetea makubaliano hayo ya kinyuklia. Li amesema kusambaratika kwa makubaliano hayo ya Iran kutahujumu pia juhudi za kuitaka Korea Kaskazini kukomesha mpango wake wa kinyuklia.

Iran yatoa masharti

Kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei leo amewahutubia maafisa wa serikali na kutoa muongozo wa masharti ambayo nchi hiyo inataka nchi zenye nguvu zaidi duniani zilizosalia katika makubaliano hayo kuyazingatia iwapo zinataka kuyanusuru.

Iran Ali Khamenei
Kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: Mehr

Ali Khamenei amesema kujiondoa kwa Marekani kutoka makubaliano hayo ni ukiukaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2231 lililopekea kufikiwa kwa makubaliano hayo na kuzitaka nchi za Ulaya kuwasilisha azimio katika baraza hilo kupinga hatua ya Marekani.

Pia amewataka viongozi wa nchi tatu za Ulaya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuahidi kutopinga ushawishi wa Iran katika kanda ya Mashariki ya Kati au kuwepo kwa mpango wake wa kinyuklia kwani kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa Iran inanuia kudumisha mpango huo kwa minajili ya kujilinda, akiahidi watarejelea shughuli zao za kutaka kuzalisha asilimia 20 ya madini ya Urani iwapo makubaliano hayo yatafeli.

Iran pia imetaka nchi za Ulaya kuahidi kuwa itanunua mafuta yake iwapo Marekani itafanikiwa kutatiza uuzaji wa mafuta kupitia kuiwekea tena vikwazo. Khamenei amesema Iran haitafuti mkwaruzano na nchi za Ulaya lakini kutokana na mienendo yake katika kipindi cha nyuma hawawezi kuwaamini na kutokana na hilo wanataka kupata hakikisho thabiti.

Mwandishi: Caro Robi

Mhariri: Yusuf, Saumu