1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yapamba moto Mashariki ya Kati

3 Julai 2014

Mamia ya Wapalestina wameandamana Jerusalem ya Mashariki kufuatia kutekwa nyara na kuuwawa kwa kijana wa Kipalestina siku mbili baada ya kupatikana kwa maiti tatu za vijana wa Israel kwenye msitu wa Ukingo wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/1CUz1
Wapalestina wakipambnana na polisi wa Israel huko Shuafat. (02.07.2014)
Wapalestina wakipambnana na polisi wa Israel huko Shuafat. (02.07.2014)Picha: Reuters

Israel imefanya mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza kabla ya alfajiriya leo kwa kuyalenga maeneo matano yakiwemo maeneo yalioficha zana za kufyetulia maroketi. Taarifa ya jeshi la Israel imesema imefanya mashambulizi hayo kufuatia kuvurumishwa kwa maroketi nchini Israel kutoka Gaza kulikofanywa na wanamgambo wa Kipalestina.

Nyumba mbili zilipigwa na maroketi katika mji wa Sderot kaskazini mashariki ya Ukanda wa Gaza na kusababisha kukatika kwa umeme katika mji huo. Vingora vya kutowa onyo vimekuwa vikisikika usiku kucha kwa wakaazi wa Israel katika eneo hilo lote.Wapalestina 11 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Israel huko Gaza na mmoja wao yuko mahtuti.

Huko Jerusalem ya Mashariki vijana kadhaa wa Kipalestina baadhi yao wakitumia panda wamewavurumishia mawe polisi wa Israel katika barabara kuu ya kuelekea Shu'afat kitongoji ambako ndiko alikotekwa nyara kijana wa Kipalestina na kuuwawa.Askari mmoja wa Israel na mfanyakazi mmoja wa matibabu walijeruhiwa na vituo vitatu vya reli viliharibiwa katika ghasia hizo za jana.

Maandamano dhidi ya ghasia

Pia Waisrael 1,000 waliandamana mjini Jerusalem nje ya makaazi ya Waziri Mkuu Banjamin Netanyahu jana usiku kupinga matumizi ya nguvu.

Mpalestina aliyejeruhiwa wakati wa mapambano na polisi wa Israel huko Shuafat.(02.07.2014)
Mpalestina aliyejeruhiwa wakati wa mapambano na polisi wa Israel huko Shuafat.(02.07.2014)Picha: Reuters

Yitzhak Herzog kiongozi wa upinzani amesema Wayahudi na Waarabu lazima waishi pamoja katika nchi hiyo na kwamba watu wenye misimamo mikali wamekuwa wakijaribu kuchochea mkondo mpya wa umwagaji damu.Lakini wengi wa Wayahudi na Waarabu wanataka kuishi kwa amani.

Mark Regev msemaji wa serikali ya Israel amekaririwa akisema "Waziri Mkuu wa Netanyahu amewaagiza polisi kufanya uchunguzi kwa makini kujuwa ukweli juu ya kuuwawa kwa kijana huyo wa Kipalestina na kuwataka watu wasijichukulie sheria mikononi mwao".

Mwili wagunduliwa msituni

Mwili wa kijana huyo Muhammad Abu Khdair mwenye umri wa miaka 16 uligunduliwa kwenye msitu wa Jerusalem hapo jana ikiwa ni siku mbili baada ya miili ya vijana watatu wa Kiisrael waliotekwa nyara na kuuwawa kugunduliwa katika msitu mmoja wa Palestina.

Polisi wa Israel wakati wa mapambano na Wapalestina huko Shuafat.(02.07.2014)
Polisi wa Israel wakati wa mapambano na Wapalestina huko Shuafat.(02.07.2014)Picha: Reuters

Ndugu wa kijana huyo wamesema alitekwa nyara wakati wa alfajiri mbele ya nyumba yao katika kambi ya wakimbizi ya Shu'afat Jerusalem ya Mashariki . Wamesema alibwakuliwa kwa nguvu na kuingizwa kwenye gari moja ambao marafiki aliokuwa nao walipojaribu kulifuata lilikimbia.

Wachambuzi wanasema kuuwawa kwa kijana huyo wa Kipalestina kutapunguza uhuru wa Israel kuchukuwa hatua dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas ambapo wanachama wake wawili wanatuhumiwa kuhusika na utekaji nyara na kuuwawa kwa vijana watatu wa Kiisrael.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri : Josephat Charo