1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa habari wapigwa risasi mguuni.

14 Mei 2010

Watu 30 wameuawa, 1400 wamejeruhiwa tangu machafuko yaanze mwezi Aprili.

https://p.dw.com/p/NNQ4
Wanajeshi nchini Thailand watuhumiwa kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji.Picha: AP

Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Reuters, alisema hakuwa na uhakika ikiwa wanajeshi walitumia risasi za kweli au zile za mipira.

Shirika la habari la Ufaransa la France 24 limedhibitisha kwamba mwandishi wa habari anayelifanyia kazi amejeruhiwa baada ya kufyatuliwa risasi mguuni alipokuwa akishughulika wakati wa machafuko karibu na eneo la Suan Lum. Mpiga picha wa Thailand wa gazeti la Matichon pia alipigwa risasi mguuni mjini Bangkok.

Wachunguzi wa kisiasa wanasema kwamba mpasuko katika jeshi ambapo wanajeshi wengine wanamuunga mkono waziri mkuu aliyeondolewa madarakani, Thaksin Shinawatra utavuruga jitihada za kudhibiti machafuko hayo.

Mwandishi wa habari wa shirika la Reuters alisema alimuona afisa mmoja wa polisi akiwafyatulia risasi wanajeshi wakati wa machafuko hayo. Msemaji wa serikali ya Thailand, Panitan Wattanayagorn aliitetea mikakati ya jeshi akisema wamefuata sheria za kimataifa.

Unruhe und Gewalt in Thailand
Waandamanaji wa mashati mekundu wakikabiliana na wanajeshi mjini Bangkok.Picha: AP
Wanajeshi bado hawajazifunga barabara zinazoingia katika eneo ambalo waandamanaji wanaovalia mashati mekundu wamepiga kambi hivyo kuzua masuali ikiwa serikali itaweza kusitisha maandamano.

Mtu mmoja aliuawa na wengine 11 kujeruhiwa katika machafuko ya tangu jana usiku ingawa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka. Hospitali nyingi zimesita kutoa idadi kamili ya majeruhi.

Mzozo huo ambao umesababisha kiasi ya watu 30 kuawa na zaidi ya wengine 1400 kujeruhiwa tangu mwezi Aprili, umevuruga shughuli katika mji mkuu wa Bangkok, umewatia uwoga wawekezaji na umeanza kuathiri pakubwa uchumi wa taifa hilo.

Nattawut Saikua ambaye ni kiongozi wa waandamanaji, akihutubia umati wa takriban watu 10,000 alisema ingawa jeshi linawazidi nguvu, hawatakata tamaa na watapigana hadi mwisho. Machafuko hayo yalikithiri baada ya agizo kali la usalama kutolewa jana jioni kuwataka waandamanaji waondoke katika eneo la kati kati ya jiji wanakopiga kambi kufuatia kusambaratika kwa mpango wa maridhiano uliopendekezwa na waziri mkuu, Abhisit Vejjajiva.

Habari za hivi punde zinasema waziri mkuu aliyeondolewa madarakani, Thaksin Shinawatra ,ambaye anaishi uhamishoni tangu alipoangushwa ameitaka serikali iwaondoe wanajeshi kutoka katika eneo linalokaliwa na waandamanaji wa mashati mekundu na ianze upya mazungumzo ya amani.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters/AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed