1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vitega uchumi-Afrika ya kusini

Nijimbere, Gregoire23 Mei 2008

Mashambulio yaliyowalenga wageni nchini Afrika ya kusini, yanaweza kuwatisha wawekezaji kutoka nje na kuelekea katika nchi nyingine za kiafrika.

https://p.dw.com/p/E53E
Umati wa raia wa kigeni walioyakimbia mashambuliziPicha: AP



Machafuko yaliyowalenga wageni nchini Afrika ya kusini yanaweza kuwatisha wawekezaji wa kigeni na kuvutiwa na nchi nyingine za kiafrika


Picha za wageni wakikimbia mauaji na visa vya mateso walivyopitishiwa na wenyeji pamoja na machafuko wakati polisi wakijaribu kuzikomesha ghasia hizo katika vitongoji, vimeongeza hofu kwa wawekezaji kutoka nje ambao tayari walikuwa na wasi wasi juu ya urithi kwenye uongozi wa nchi, kukatikakatika umeme, mfumuko wa bei na matatizo mengine yanayoikabili nchi hiyo ya Afrika ya kusini licha ya kuwa ya kwanza kiuchumi barani Afrika.

" Hili ni pigo jingine japokuwa singeshauri watu kuingiwa na wasi wasi wakati huu", amesema mtaalamu katika shirika la BNP Paribas Elizabeth Gruie kabla ya kuongeza "tunasubiri kuona mnamna serikali itakavyoyashughulikia maswala yote hayo kwa muda mfupi ujao, mnamna hiyo inaweza kubadili misimamo katika nchi nyingine za kiafrika lakini hata hivyo yaonyesha bado uchumi umekuwa tu".

Mwezi uliopita, Fuko la fedha la kimataifa IMF,

lilisema linatarajia uchumi utakuwa kwa asili mia 6,5 barani Afrika mwaka huu, ikiwa ni chini kidogo na kiwango cha mwaka uliopita cha asili mia 6,6 licha ya mikopo kutotolewa vizuri na matatizo ya kiuchumi nchini Marekani.

Na ni wiki iliopita tu, shirika la kodi la Standard and Poor lilisema kuwa, ughali wa huduma na ustawi wa uchumi vitaimarisha kukuwa kwa uchumi katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na kuilinda sehemu hiyo ya Afrika na matatizo ya kiuchumi katika nchi za magharibi, hali haitokuwa hivyo kwa nchi ya Afrika ya kusini, ambayo tayari salafu yake imeshuka thamani kwa kiwango fulani kutokana na machafuko dhihi ya wageni.

Mbali na hayo wawekezaji bado wanashakashaka kuhusu sera za Jacob Zuma iwapo atachukuwa madaraka ambazo kwa maoni yao si wazi. Baadhi yao wanahisi kuwa iwapo atachaguliwa, anaweza kuongeza matumizi ya serikali kupita kiasi na kuvuruga uchumi wa taifa. Matamshi yake dhidi ya rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, yaliwatia moyo wana uchumi lakini wanasubiri kuona ni upi utakuwa msimamo wake juu ya ghasia za hivi karibuni dhidi ya wageni.

Wakati kiwango cha uwekezaji kikishuka huko nchini Afrika ya kusini, fedha zimezidi kumiminika katika nchi nyingine za bara la Afrika ambako wawekezaji wanasema hali ya kisiasa imetengamaa, mawasiliano mazuri kwa kuibuka mfumo wa simu za mikononi na miundo mbinu nzuri vile vile.

Miongoni mwa nchi zimeonekana tulivu kisiasa na kuvutia zaidi ni pamoja na Ghana,Tanzania na Zambia.

Kenya baada ya kujikwamua kutoka lindi la machafuko yaliyofuatia uchaguzi wa mwaka jana, imeanza kushuhudia wawekezaji wakirudi. Wawekezaji hao hawawezi kuiacha nyuma pia Nigeria kutokana na mafuta yake licha ya kukabiliwa na hali ya vurugu kisiasa na kiuchumi na kuwa hatari kiusalama.

Mnamo siku hizi, China, nchi na mashirika mengine ya wawekezaji kutoka Eshia, bila kusahau mashirika ya watu binafsi kutoka nchi za magharibi wameongeza maradufu shughuli zao barani Afrika na hivyo kuchangia kukuuza uchumi wake. Kulingana na takwim zilizotolewa mwaka 2006, kiwango cha uwekezaji katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kilifikia bilioni 2,3 dala za kimarekani.

Baadhi ya watu wanaona kuwa matumaini uchumi wa Afrika kuzidi kukuwa yanategemea China na kupungua kwa nafasi ya nchi za magharibi. Wengine wanahisi kuwa kwa vyovyote vile, uchumi wa bara la Afrika bado uko katika hali nzuri kuweza kuendelea kukuwa.