1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabishano juu ya wakimbizi wanaokuja Ulaya

Maja Dreyer12 Juni 2007

Idadi ya wakimbizi wa kutoka Afrika wanaofika kwenye fukwe za pwani za bara la Ulaya inabakia kuwa kubwa. Wikiendi iliyopita pekee, Waafrika 300 walifika kwenye visiwa vya Canaries. Ndiyo sababu, mawaziri wa ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wamezungumzia tatizo hilo kwenye mkutano wao leo hii. Kwa kweli, ni suala ambalo linazusha mvutano kati ya nchi wanachama wa Umoja huu.

https://p.dw.com/p/CHCk
Wakimbizi kwenye boti
Wakimbizi kwenye botiPicha: AP

“Ikiwa mtu anataraji kisiwa hiki kidogo kitachukua wakimbizi waliookolewa nje ya eneo tunalodhibiti, hili haliwezekani.”

Anayesema hayo ni Tonio Borg, waziri wa mambo ya ndani ya Malta, taifa la kisiwa kiliopo kusini mwa Italia kati ya bara la Ulaya na la Afrika. Kwenye mkutano na mawaziri wenzake wa Umoja wa Ulaya, Bw. Borg alizilaumu nchi nyingine za Umoja huu kwa kutoisaidia Malta katika masuala ya wakimbizi.

Ili kuonyesha uzito wa tatizo hilo kisiwani Malta, waziri Borg anatoa mfano: “Kwa mfano, mwaka uliopita tumechukua wakimbizi elfu mbili. Tukihamisha idadi hii sambamba na idadi ya raia wa Ujerumani, ni kama Ujerumani ingechukua wakimbizi 400.000. Sasa ufikirie tu vile hali hiyo ingesababisha mzozo mkubwa huko Ujerumani.”

Kwa sababu hiyo, waziri Borg alitoa pendekezo kwenye mkutano wa leo mjini Brussels, Ubelgiji, kuwa wakimbizi wanaokolewa kutoka meli zao au wanaofika kwenye nchi za bahari Kusini mwa Ulaya wapelekwe kwenye nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya ili kuugawa mzigo huo. Mawaziri wengine kadhaa walikataa pendekezo hilo wakiwemo pia mawaziri wa Spain na Italia. Hao wanahofia hatua kama hiyo ingesababisha idadi ya wakimbizi kuzidi. Badala yake, mawaziri hao wanadai, idara inayoshughulikia kulinda mipaka ya Ulaya ifanye bidii kubwa zaidi meli zisitoke kutoka pwani za bara la Afrika.

Malta inakabiliwa na tatizo hilo hasa kwa sababu licha ya kuwa nchi ndogo inadhibiti eneo kubwa la bahari. Kulingana na sheria za bahari, wakimbizi wanapaswa kuokolewa na kuchukuliwa na nchi husika inayodhibiti eneo husika la bahari. Waziri Borg wa Malta alilalamika pia juu ya idadi kubwa ya wakimbizi wanaozama kwa sababu nchi husika hazitekelezi jukumu lao la kuwaokoa.

Juu ya suala la wakimbizi, mawaziri wa ndani wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wao wa leo wamekubaliana kubadilishana mafaili ya wahalifu au watuhumiwa wa polisi ili kurahisisha kazi za kuwatafuta wahalifu hao barani Ulaya. Ushirikiano huo wa idara za mipaka utahitajika kuanzia mwisho mwa mwaka huu ambapo udhibiti wa mipaka kati ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya utaondoshwa. Wakati huo huo, nchi za Umoja wa Ulaya zitakuwa na data za pamoja za kukusanya habari zote kuhusiana na visa, yaani ruhusu za kuingia nchini zinazotolewa na nchi za Umoja huo.